Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata raia wanne wa China wanaotuhumiwa kuhusika katika tukio la utekaji wa wafanyabiashara wenzao kutoka nchini humo, huku wakidai kiasi cha dola za Marekani milioni 20 ili kuwaachia huru.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 25, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, alisema tukio hilo lilitokea Mei 14 majira ya saa 4:30 usiku katika majengo ya PSSSF yaliyopo Mtaa wa Mission, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, kundi la watu saba wanaodaiwa kuwa wahalifu liliwavamia na kuwateka wafanyabiashara hao wawili ambao ni Weiyi Chen (64) na Liang Xiolo (44), kabla ya kuwapeleka katika eneo lisilojulikana na kuanza kudai fedha kwa ajili ya kuwaachia.

Katika operesheni ya msako iliyofanywa na Polisi, magari mawili yanayodaiwa kutumika katika tukio hilo yalikamatwa, yakiwemo Toyota Alphard yenye namba za usajili wa kubuni T.305 DRP pamoja na Toyota Harrier yenye namba T.188 DHT.

Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwaokoa wahanga hao Mei 16, 2026 katika eneo la Mbezi, Wilaya ya Kinondoni,Maeneo ya Mbezi wakiwa wamejeruhiwa.

Wahanga hao walipelekwa katika Hospitali ya Agha Khan kwa ajili ya matibabu, ambapo hali ya Weiyi Chen imeelezwa kuwa mbaya huku mwenzake akiendelea kupata huduma za kitabibu.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Deng Anqing (49), Fan Zhong (49), Zhang Jianjun (51), na Deng Qiang (40), ambao walikutwa na simu zinazodaiwa kuwa za wahanga pamoja na vielelezo vingine vinavyoendelea kufanyiwa uchunguzi.

Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea huku likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na uhalifu huo.