Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)limetangaza ongezeko kubwa la nafasi za vijana watakaopatiwa mafunzo ya uzalendo na stadi za maisha mwaka huu, ambapo wahitimu wa kidato cha sita wapatao 60,000 wanatarajiwa kuripoti katika makambi mbalimbali nchini kuanzia Juni 1, 2026.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuendelea kuwajengea vijana uzalendo, nidhamu, uwezo wa kujitegemea pamoja na kuwapa ujuzi utakaowasaidia katika maisha ya baadae.

Akizungumza leo Mei 28,2026 Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema idadi hiyo imeongezeka kutoka vijana 40,000 waliokuwa wakichukuliwa hapo awali hadi kufikia 60,000 mwaka huu.

Amesema vijana waliochaguliwa wanatoka katika shule mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar, huku wakitakiwa kuripoti katika makambi waliopangiwa ndani ya kipindi cha Juni 1 hadi Juni 7 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mabena, Serikali inalenga kuona mfumo huo unakuwa endelevu ili wahitimu wengi zaidi wa elimu ya sekondari waweze kupitia mafunzo hayo muhimu kwa maendeleo ya taifa na kujijengea uwezo binafsi.

Ametaja baadhi ya kambi zitakazopokea vijana hao kuwa ni pamoja na Rwamkoma mkoani Mara, Msange Tabora, Mpwapwa na Makutupora Dodoma, Mafinga Iringa, pamoja na Oljoro Arusha.

Kambi nyingine ni Bulombora Kagera, Kanembwa na Mtabila Kigoma, Itaka Songwe, Luwa na Milundikwa Rukwa pamoja na Nachingwea Lindi.

Aidha, vijana wenye mahitaji maalum ya ulemavu wa viungo wametakiwa kuripoti katika Kambi ya Ruvu, mkoani Pwani kutokana na uwepo wa mazingira rafiki na miundombinu inayoweza kuwahudumia.

JKT pia limetoa maelekezo kuhusu vifaa muhimu vinavyopaswa kubebwa na vijana hao, ikiwemo mavazi ya michezo, shuka, soksi pamoja na nyaraka muhimu za masomo na utambulisho.

Amesisitiza kuwa mafunzo hayo siyo tu ya kijeshi bali yanakusudia kuwajenga vijana kuwa wazalendo, wenye nidhamu na uwezo wa kujitegemea hata kwa wale ambao hawatapata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu.

Programu ya mafunzo ya lazima ya JKT ilirejeshwa rasmi mwaka 2013 baada ya kusitishwa kwa muda mrefu, ikiwa na lengo la kuimarisha uzalendo na ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo ya taifa.