Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO),imetangaza rasmi ushirikiano wa Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu changamoto za matukio ya hali mbaya ya hewa, na utoaji wa tahadhari za mapema, na usalama kwenye maji hapa Tanzania.

Akizungumza leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden,Jijini Dar -Es -Salaam,Afisa Uchechemuzi (Advocacy Officer) kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO),Mary Mahemba,alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuifikia jamii kwa taarifa sahihi zinazoweza kusaidia kuokoa maisha, kupunguza athari za majanga yanayohusiana na hali ya hewa, pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu usalama majini.

“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga. Kupitia tuzo hizi tunatambua mchango wao katika kujenga jamii salama na inayotambua hatari za kuzama maji,” amesema

Mahemba amesema tuzo hizo zinalenga kuhamasisha utayarishaji wa habari zenye ubora kuhusu,Matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake kwa jamii,Tahadhari za mapema za hali ya hewa,Usalama wa vyombo vya usafiri na usafirishaji kwenye maji,Uzuiaji wa ajali na vifo vitokanavyo na kuzama maji,Ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,Meneja Masoko na Uhusiano,Monica Mutoni,amesisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema katika kuokoa maisha ya wananchi, hususan wale wanaotegemea shughuli za maji kama vile uvuvi na usafiri wa majini.

Mutoni amesema, TMA imeendelea kuhakikisha mchango wa wanahabari utambulika kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa kuongeza thamani za Tuzo za Wanahabari wa Masuala ya Hali ya Hewa nchini. ”Ushirikiano katika tuzo hizi ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari katika kuimarisha uelewa, usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii,”amesema

Kwa muktadha huu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la EMEDO wameandaa Tuzo zitakazowahusisha waandishi wa Habari.

Tuzo hizo zitahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.

Ambapo waandishi wanaalikwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agost mosi,2025 mpaka Agost 30,2026.