Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imewataka viongozi wa mikoa na wilaya, hususan maeneo ya mipakani, kuongeza usimamizi wa mbegu zinazoingia nchini ili kuzuia kuenea kwa mbegu zisizo na ubora ambazo zimekuwa zikichangia hasara kwa wakulima na kudhoofisha sekta ya kilimo.
Maagizo hayo yametolewa Leo Mei 28,2026 Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu 2026 uliofanyika jijini Dodoma.
Amesema Serikali haitavumilia uingizaji wa mbegu holela kupitia mipaka ya nchi kwani hali hiyo imekuwa ikiathiri juhudi za kuongeza uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula nchini.
“Wakulima wanapopata mbegu zisizo bora, lawama zote zinaielekea serikali, ni lazima mifumo ya ukaguzi iimarishe ufanisi wake,” amesema.
Katika hatua nyingine, Silinde amewataka wazalishaji wa mbegu nchini kuwekeza zaidi katika teknolojia ya kuzalisha mbegu zinazostahimili ukame na magonjwa ili kusaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Serikali inalenga kuona Tanzania inapunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje kwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani, sambamba na kuimarisha sekta ya viwanda vya kilimo.
Aidha, amewataka wadau wa kifedha kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wakulima na wazalishaji wa mbegu kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo cha kisasa.
Silinde amesema sekta ya mbegu inahitaji uwekezaji mkubwa katika maeneo ya umwagiliaji, uhifadhi na uchakataji ili kuongeza uzalishaji wenye tija.
Pia amewataka viongozi wa serikali za mitaa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora, akieleza kuwa baadhi ya wilaya tayari zimeanza kuchukua hatua hiyo kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ASPIRES Tanzania, Profesa David Nyange amesema matumizi ya mbegu bora nchini bado ni madogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya wakulima.
Amesema kiwango cha matumizi ya mbegu bora nchini bado hakijaridhisha huku matumizi ya mbegu za kisasa aina ya hybrid yakiwa chini ya matarajio.
“Bado tunahitaji kuongeza elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora ili kuongeza uzalishaji na kipato,” amesema.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Justina Rahi alisema uzalishaji mdogo wa mbegu bora unapaswa kupewa kipaumbele ikiwa taifa linataka kuhakikisha usalama wa chakula katika miaka ijayo.
Amesema pamoja na mahitaji ya mbegu kuongezeka kila mwaka, uzalishaji wa ndani bado haujakidhi kiwango kinachohitajika na hivyo kuwataka wadau kushirikiana kuongeza upatikanaji wa mbegu kwa bei nafuu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Official Seed Certification Institute (TOSCI), Nyasebwa Chimagu amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na serikali kuhakikisha ubora wa mbegu unaimarishwa kwa maslahi ya wakulima na taifa kwa ujumla.






