Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo Mei 28, 2026 limetambua mchango mkubwa wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) katika kuandika na kuhabarisha umma kuhusu masuala ya utunzaji wa mazingira kwa weledi na umahiri mkubwa.

Utambuzi huo umetolewa kupitia tuzo maalum ya umahiri iliyokabidhiwa kwa Mkurugenzi wa JET, John Chikomo, ikiwa ni sehemu ya kuthamini kazi kubwa inayofanywa na waandishi wa habari za mazingira nchini katika kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Chikomo amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa wanachama wote wa JET na ni uthibitisho kuwa kazi inayofanywa na waandishi wa habari za mazingira inatambuliwa na serikali pamoja na wadau wa mazingira nchini.

“Leo tumetunukiwa tuzo ya umahiri kutoka NEMC kwa kutambua mchango mkubwa ambao JET imekuwa ikiutoa tangu kuanzishwa kwake.

Hii inaonesha kuwa mchango wa waandishi wa habari za mazingira katika kuhamasisha na kuhabarisha umma kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira unatambuliwa,” amesema Chikomo.

Ameeleza kuwa tangu miaka ya mwanzo ya uanzishwaji wa sera za mazingira nchini, JET imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taarifa za mazingira zinawafikia wananchi kupitia magazeti, redio na televisheni.

Kwa mujibu wa Chikomo, tuzo hiyo haipaswi kuchukuliwa kwa wepesi kwani ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa kwa muda mrefu na wanachama wa JET kwa kushirikiana na sekretarieti ya chama hicho.

“Tuzo hii si ya ofisi pekee, bali ni ya wanachama wote wa JET ambao wamekuwa bega kwa bega kuhakikisha habari za mazingira zinaandikwa kwa weledi mkubwa.

“Kazi yao haiendi bure kwa sababu serikali na wadau mbalimbali wametambua mchango wao,” amesema.

Aidha, amesema kutambuliwa huko kunapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi zaidi katika kuandika habari za mazingira kwa umakini na weledi ili kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kulinda mazingira.

Chikomo amesema JET, ambayo sasa inaelekea kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, inaona hatua hiyo kama mwanzo mpya wa mafanikio makubwa zaidi katika sekta ya habari za mazingira.

“Wanasema maisha yanaanza miaka 40. Sisi JET tunaona sasa ndiyo tunaanza upya kwa nguvu kubwa zaidi katika kuhakikisha tunasogeza mbele gurudumu la uhifadhi wa mazingira nchini,” amesema.

JET ambayo imekabidhiwa tuzo hiyo na Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba kwenye siku ya kwanza ya maadhimisho ya kilele cha miaka 40 ya NEMC, imeendelea kuwa taasisi muhimu inayowaunganisha waandishi wa habari za mazingira nchini huku ikichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu changamoto za mazingira, mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali za asili.