Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetoa wito kwa vijana wote waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita 2026 kutoka shule za Tanzania Bara na Zanzibar kuripoti kwenye makambi mbalimbali ya JKT kwa ajili ya Mafunzo ya JKT Kundi la lazima kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Makao Makuu ya JKT mkoa Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena alisema vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Juni mosi hadi Juni saba mwaka 2026.
Alisema vijana hao wamepangiwa katika makambi mbalimbali nchini ikiwemo Rwamkoma JKT mkoani Mara, Msange JKT-Tabora, Ruvu na Kibiti JKT-Pwani, Mpwapwa na Makutupora JKT-Dodoma, Mafinga JKT-Iringa, Mlale JKT-Ruvuma, pamoja na makambi mengine yaliyopo Tanga, Arusha, Kigoma, Songwe, Rukwa, Lindi na Dar es Salaam.
Brigedia Jenerali Mabena amewataka wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho kuripoti katika Kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwahudumia.
Aidha, JKT limewataka vijana hao kuripoti wakiwa na vifaa muhimu ikiwemo bukta ya dark blue, T-shirt ya kijani, raba za michezo, shuka mbili za blue bahari, soksi nyeusi, track suit pamoja na nyaraka zote muhimu za masomo ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vya kuhitimu kidato cha nne na sita.
Brigedia Jenerali Mabena alisema orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa, makambi waliopangiwa pamoja na maelekezo mengine inapatikana kupitia tovuti rasmi ya JKT ambapo wahitimu watatakiwa kuingiza jina la shule au namba ya shule ili kuona kambi walizopangiwa.
Amewakaribisha vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2026 kujiunga na mafunzo hayo kwa lengo la kujengewa uzalendo, nidhamu, ukakamavu, umoja wa kitaifa pamoja na stadi mbalimbali za maisha na kazi kwa ajili ya kulitumikia Taifa.


