Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, alisimama kwa muda kando ya kitanda cha binti mdogo Catherine P. Conrdad Minja mwenye umri wa miaka minne katika Taasisi ya Mifupa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI), akimsabahi na kumtakia nafuu ya haraka baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mapema wiki hiyo, akiwa mmoja wa wagonjwa wa mwanzo kufanyiwa upasuaji huo katika Taasisi hiyo.
Jioni ya Ijumaa Mei 29, 2026 – yaani leo Rais huyo mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana kwa mara nyingine na Catherine P. Conrad Minja ambaye Julai 19 mwaka huu atatimiza umri wa miaka 22 , ikiwa ni miaka 18 toka walipoonana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mapema wiki hiyo.
Catherine hivi sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza akisomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Kairuki jijini Dar es salaam, alifika ofisini kwa Rais Mstaafu kumsabahi na kumshukuru kwa juhudi zake za kuanzisha na kusimamia taasisi za magonjwa ya moyo.
Dkt. Kikwete amempongeza Catherine kwa kuchagua masomo ya udaktari kama alivyomuahidi miaka 18 iliyopita, na amefurahi kumuona mmoja wa wagonjwa wa kwanza kufanyiwa upasuaji Taasisi ya MOI ambayo ni moja ya taasisi za rufaa zinazoongoza Afrika Mashariki katika kushughulikia kesi ngumu za magonjwa na majeraha ya mifupa, misuli, viungo, ubongo na mfumo wa fahamu.
Catherine amemwambia Rais Mstaafu kwamba angependa kuwa Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo huko mbeleni, ili asaidie watu wenye shida hiyo iwe kama shukrani zake kwa Mungu kwa kuwezesha apone na kuendelea kuishi.





