Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dodoma
MKURUGENZI mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binasi (PPPC) , David Kafulila, amesema lengo la Serikali la kufikia uchumi wa dola trillion moja ifikapo mwaka 2050 haliwezi kufikiwa ikiwa Watanzania hawatabadilika kifikra na kuongeza maarifa.
Kafulila alisema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayatategemea ukubwa wa rasilimali zilizopo nchini pekee, bali ubora wa rasilimali watu na uwezo wao wa kutumia maarifa na teknolojia kuzalisha matokeo yenye tija kwa uchumi.
Akizungumza katika Muhadhara wa Umma ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Kafulila alisema Tanzania inalenga kufikia uchumi wa dola trilioni moja ambao utamwezesha kila Mtanzania kuwa na wastani wa pato la takribani dola 7,000 kwa mwaka.
“Dunia ya sasa haishindani kwa mali au rasilimali ilizonazo. Ushindani uliopo ni wa ubora wa watu na uwezo wao wa kuleta matokeo. Hivyo, kama tunataka kufikia uchumi wa dola trilioni moja, lazima tuwe na watu wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia,” alisema.
Alisema dunia imeingia katika enzi ambayo taarifa na teknolojia ya mawasiliano zimekuwa rasilimali muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii, huku maendeleo ya akili mnemba yakiongeza kasi ya upatikanaji wa taarifa na maarifa.
Kafulila alisema ingawa lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni moja linaonekana kubwa, bado linawezekana kufikiwa ndani ya miaka 25 iliyobaki kuelekea mwaka 2050 iwapo nchi itawekeza zaidi katika elimu, ujuzi na uzalishaji wenye tija.
Alionya kuwa ongezeko la idadi ya watu linaweza kuwa fursa au changamoto kwa maendeleo ya taifa kutegemea namna wananchi hao watakavyowezeshwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji.
“Watu wanaweza kuongezeka na kuongeza uchumi, lakini pia wanaweza kuwa mzigo kwa uchumi. Kuna watu ambao ni rasilimali na kuna ambao ni mzigo. Kazi ya vyuo vikuu ni kuwabadilisha watu kutoka kuwa mzigo kwenda kuwa rasilimali,” alisema.
Katika muhadhara huo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Razack Lokina, alisema ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema Tanzania inakabiliwa na mahitaji makubwa ya uwekezaji katika miundombinu ya umma ikiwemo barabara, bandari, masoko, nishati na huduma za afya, ambayo hayawezi kugharamiwa na Serikali pekee kwa kutumia rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa Profesa Lokina, ushiriki mkubwa wa sekta binafsi kupitia miradi ya ubia utaisaidia nchi kupata rasilimali za ziada za kifedha, utaalamu na teknolojia zinazohitajika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema majadiliano yaliyoanzishwa kupitia muhadhara huo yanatarajiwa kutoa mapendekezo ya kisera na kimkakati yatakayosaidia kuimarisha mifumo ya kisheria, kiutawala na kifedha ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi nchini.



