Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam
CRDB Benki imezindua bidhaa mpya ya mikopo kwa waajiriwa wa Serikali itakayopatikana kwa njia ya kidigitali, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wateja popote walipo kupitia simu zao za mkononi.
Akizungumza leo Juni 3, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya miezi mitatu ya “Kopa Kimpango Wako”, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa CRDB Benki, Stephen Adili, amesema huduma hiyo itaanza kutolewa rasmi kuanzia kesho, ikiwa ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuwafikia waajiriwa wa Serikali kwa urahisi zaidi.
Adili amesema kampeni hiyo inawahusu watumishi wote walioajiriwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku lengo kuu likiwa ni kuwawezesha kuboresha maisha yao kiuchumi kupitia mikopo yenye masharti nafuu na inayopatikana kwa haraka.
Ameeleza kuwa benki hiyo imefanya maboresho makubwa katika huduma za mikopo kwa kuongeza muda wa marejesho kutoka miaka 10 hadi 12, kuongeza kiwango cha juu cha mkopo kutoka Sh. milioni 200 hadi Sh. milioni 300, pamoja na kupunguza riba kutoka asilimia 17 hadi asilimia 16.
“Kila anayekopa tumeongeza muda wa marejesho kutoka miaka 10 hadi 12, ukomo wa kukopa umeongezeka kutoka Sh. milioni 200 hadi Sh. milioni 300 huku riba ikishushwa kutoka asilimia 17 hadi asilimia 16. Haya yote ni mapinduzi ya huduma ukiwa na CRDB Benki,” amesema Adili.
Aidha, amebainisha kuwa CRDB Benki inaendelea kutoa mikopo ya kununua na kukarabati nyumba, ambapo kiwango cha juu cha mkopo huo kimeongezwa kutoka Sh. bilioni 1 hadi Sh. bilioni 3. Mikopo hiyo ina muda wa marejesho wa hadi miaka 20 na riba ya asilimia 14.
Adili amewahimiza waajiriwa wa Serikali kuitumia fursa hiyo ya kampeni ya miezi mitatu ili kujikwamua kiuchumi na kutimiza malengo yao mbalimbali ya maendeleo.
“Waajiriwa wa Serikali tambueni kuwa kampeni hii isikupite. CRDB Benki tumefika mkononi mwako kupitia simu yako ya mkononi, na sasa unaweza kupata mkopo wa hadi Sh. bilioni 3.
Dhamana ni ajira yako na mwajiri wako. Chukua hatua ya kuboresha maisha yako kupitia huduma hizi mpya,” amesema.
Kampeni ya “Kopa Kimpango Wako” inatarajiwa kuendeshwa kwa miezi mitatu nchini kote, ikilenga kuwafikia maelfu ya watumishi wa umma na kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi zaidi kupitia mifumo ya kidigitali.






