Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Wamiliki wa vyombo vya majini nchini wametakiwa kutoa taarifa na takwimu sahihi wakati wa utekelezaji wa Sensa ya Vyombo vya Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa za kuaminika zitakazosaidia kupanga na kuendeleza sekta ya usafiri wa majini pamoja na kukuza uchumi wa bluu.
Wito huo umetolewa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa Leo June 3,2026 jijini hapa, wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wakala wa Usimamizi wa Meli Tanzania (TASAC), yaliyofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Msengwa amesema sensa hiyo ni hatua muhimu kwa taifa kwani itasaidia upatikanaji wa takwimu rasmi, sahihi na zenye kuaminika kuhusu vyombo vya majini na shughuli za ujenzi wa meli, ambazo zitakuwa msingi wa maamuzi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zinazohusiana na usafiri wa majini.
Amesema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za maji zikiwemo bahari, maziwa makubwa na mito, hivyo sensa hiyo itatoa picha halisi ya idadi, aina na hali ya vyombo vinavyotumika katika maeneo hayo pamoja na kubaini fursa zilizopo za uwekezaji.
“Sensa hii itatusaidia kupata takwimu bora za vyombo vinavyofanya kazi katika bahari, maziwa na mito yetu. Takwimu hizi zitasaidia Serikali na wadau mbalimbali kubaini maeneo yenye fursa za uwekezaji na kuboresha usafirishaji fungamanishi,” amesema.
Ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkazo katika kuimarisha mfumo wa usafirishaji fungamanishi, hivyo matokeo ya sensa hiyo yatatoa mwanga kuhusu maeneo yanayohitaji uwekezaji na maboresho ili kuongeza ufanisi wa sekta ya usafiri wa majini.
Kwa mujibu wa Dkt. Msengwa, maandalizi yote ya sensa hiyo yamekamilika na wataalamu wameandaliwa kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia viwango na taratibu za kitaalamu ili kupata matokeo yenye ubora unaotakiwa.
“Tunawaomba wamiliki wa vyombo vya majini kutoa taarifa sahihi kwa sababu ubora wa takwimu utakaochukuliwa ndio utakaowezesha kupatikana kwa matokeo chanya yatakayosaidia maendeleo ya sekta hii,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohammed Salum, amesema ushirikiano kati ya NBS na TASAC unaonesha dhamira ya kuendesha sekta ya usafiri wa majini kwa kutumia takwimu sahihi na za kisasa.
Amesema sensa hiyo ni mwendelezo wa zoezi la kwanza lililofanyika mwaka 2021 ambalo lilijikita zaidi katika vyombo vidogo vya majini, huku sensa ya sasa ikihusisha vyombo vya aina zote pamoja na wajenzi wa meli nchini.
“Sensa ya mwaka 2021 ilitupatia taarifa muhimu zilizotusaidia kuboresha huduma, usimamizi wa sheria na mipango ya maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini. Safari hii tunalenga kupata taswira kamili zaidi ya sekta nzima,” amesema.
Amefafanua kuwa matokeo ya sensa iliyopita yaliwezesha TASAC kuongeza wigo wa usimamizi wa vyombo vya majini kutoka takribani 6,000 hadi zaidi ya 21,600 vinavyofikiwa na kusimamiwa kwa sasa.
Aidha, amesema takwimu hizo zimeisaidia taasisi hiyo kuimarisha hoja za kuongeza rasilimali watu, kuboresha huduma za ukaguzi na usimamizi wa vyombo vya majini pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni za usalama.
Mohamed amesema lengo kuu la sensa hiyo ni kukusanya takwimu sahihi zitakazosaidia kutambua idadi na aina ya vyombo vya majini vilivyopo nchini, kiwango cha uzingatiaji wa sheria na kanuni za usalama pamoja na kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo.
“Sensa hii itatuwezesha kuwa na takwimu kamili za vyombo vya majini nchini, kusaidia mipango ya maendeleo, uwekezaji na kukuza uchumi wa bluu,” amesema.
Ameongeza kuwa matokeo ya sensa yanatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, kuvutia uwekezaji zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia matumizi bora ya rasilimali za maji zilizopo nchini.




