Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam
CRDB Foundation imezindua rasmi msimu wa 13 wa mashindano ya mpira wa miguu ya iMbeju Ndondo Cup 2026 kwa kutenga zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya uendeshaji wa mashindano hayo na zawadi mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuibua vipaji vya vijana na kuwawezesha kiuchumi kupitia michezo.
Mashindano ya mwaka huu yanakwenda na kaulimbiu ya “Jiongeze”, yakilenga kuwahamasisha vijana kutumia michezo kama chachu ya maendeleo, ajira na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliipongeza CRDB Foundation kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya vijana kupitia michezo.
Alisema Ndondo Cup imekuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji, kuimarisha mshikamano wa jamii na kutoa burudani kwa wananchi, huku ikiwajengea vijana uwezo wa kutumia vipaji vyao kujiletea maendeleo.
Mtambule aliwahamasisha vijana kutumia fursa zinazotolewa na CRDB Foundation kwa kujiunga katika vikundi vya kiuchumi vinavyoweza kuwawezesha kupata mikopo na kuanzisha shughuli za maendeleo.
“Maendeleo ya vijana yanahitaji ubunifu, nidhamu na matumizi sahihi ya fursa zilizopo. Mashindano haya ni zaidi ya mpira wa miguu, ni darasa la maisha na maendeleo,” alisema Mtambule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tuliesther Mwambapa, alisema taasisi hiyo imeendelea kuwa kinara wa uwezeshaji wa vijana na jamii kupitia programu ya Imbeju, ambayo hadi sasa imewafikia zaidi ya Watanzania milioni 1.7 katika sekta mbalimbali.
Alieleza kuwa kupitia programu hiyo, zaidi ya shilingi bilioni 23 zimetolewa kama mikopo nafuu kwa vijana na vikundi vyao, hatua iliyowasaidia wengi kujikwamua kiuchumi.
Mwambapa alisema Ndondo Cup si mashindano ya mpira wa miguu pekee bali ni jukwaa la kuibua vipaji, kujenga ajira na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za maendeleo.
“CRDB Foundation imetenga zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya Ndondo Cup 2026. Kati ya fedha hizo, zaidi ya shilingi milioni 100 zitatolewa kama zawadi kwa washiriki katika hatua mbalimbali za mashindano.
Bingwa wa mwaka huu atajinyakulia shilingi milioni 30 pamoja na timu nzima kulipiwa safari ya kwenda kushuhudia michuano ya AFCON. Mshindi wa pili atapata shilingi milioni 20,” alisema Mwambapa.
Aliongeza kuwa mchezaji bora atazawadiwa shilingi milioni 3, huku mfungaji bora, beki bora na kipa bora kila mmoja akiondoka na shilingi milioni 1.
Katika hatua nyingine, Mwambapa alisema kombe la Ndondo Cup 2026 litakuwa na hadhi ya kimataifa, likiwa tayari limebuniwa na kutengenezwa nchini China ili kuongeza thamani na heshima ya mashindano hayo.
Aidha, Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na waandaaji wa mashindano hayo kwa kuhakikisha usalama unaimarishwa katika viwanja vyote vitakavyotumika, ili mashindano yafanyike katika mazingira salama na yenye ushindani wa hali ya juu.
Uzinduzi wa iMbeju Ndondo Cup 2026 unatarajiwa kuibua ushindani mkubwa miongoni mwa timu za mitaani, huku maelfu ya vijana wakipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kufungua milango ya mafanikio ndani na nje ya Tanzania.




