Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma
Makamu wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi ameagiza kuwa kila kibali cha ujenzi kitakachotolewa nchini lazima kihusishe upandaji wa angalau miti mitano, ikiwa ni sehemu ya hatua mpya za kuimarisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Dk. Nchimbi ametoa maelekezo hayo leo Juni 5, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Jijini Dodoma, akisisitiza kuwa mamlaka zote za serikali, taasisi na wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan ,Nchimbi amesema pamoja na sharti la upandaji miti katika ujenzi, Manispaa na Majiji yote yanapaswa kuhakikisha kila mji unakuwa na bustani za kijani zinazotunzwa ipasavyo ili kuboresha mazingira ya makazi na kupunguza athari za ongezeko la joto duniani.
Aidha, ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha upatikanaji wa miche ya miti ya kutosha ili kuwezesha utekelezaji wa kampeni za upandaji miti nchini.
Pia ameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha misitu yote inayostahili inasajiliwa kwa ajili ya kuhifadhi hewa ukaa, huku Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikitakiwa kuimarisha usimamizi wa mipango miji ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaotokana na ukuaji holela wa makazi.
Dk. Nchimbi amesema mamlaka za serikali za mitaa zinapaswa kuwekeza katika tafiti zitakazosaidia kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili mifugo na wanyamapori kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesisitiza kuwa suala la mazingira ni ajenda ya kimataifa isiyotambua mipaka ya nchi, hivyo linahitaji ushiriki wa kila mtu katika kuhakikisha rasilimali za asili zinatunzwa kwa uendelevu.
“Tunapaswa kuchukua hatua sasa kwa sababu mazingira ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuongezeka na zinahitaji majibu ya pamoja kutoka kwa kila sekta,” amesema.
Makamu wa Rais amesema ukuaji wa idadi ya watu nchini unaongeza umuhimu wa kuimarisha mikakati ya utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinaendelea kukidhi mahitaji ya wananchi katika miaka ijayo.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema Serikali imezindua Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania itakayoweka msingi wa ushirikiano mpana katika uhifadhi wa mazingira.
Amesema programu hiyo itawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi za umma, sekta binafsi, mashirika na wananchi kwa lengo la kuimarisha juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi nchini.








