Na Deodatus Balile, Moscow, Russia
Wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya ziara ya kiserikali katika Shirikisho la Urusi kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026. Ziara hiyo imekuja miaka 57 baada ya ziara rasmi ya mwisho ya viongozi wakuu wa nchi kati ya Tanzania na Urusi, na ilikuwa ziara ya kwanza ya aina hiyo kufanyika kwa Rais wa Tanzania tangu ile ya kihistoria ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1969.
Ziara hii imempa Rais Samia fursa ya kufanya mazungumzo rasmi ya pande mbili na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin, katika Ikulu ya Urusi, ijulikanayo kama Kremlin. Pamoja na shughuli nyingine, Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Honoris Causa) na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi, kinachojulikana pia kama Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba (RUDN). Hii ni shahada ya nane ya heshima kwa Rais Samia ndani ya kipindi cha miaka sita.
Lengo kuu la ziara lilikuwa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia kati ya Tanzania na Urusi. Katika mazungumzo yao Kremlin, viongozi hao wawili wamejadili kuimarisha uhusiano wa nchi hizi rafiki, masuala ya kimataifa na kikanda, pamoja na maandalizi ya ushirikiano endelevu kati ya Urusi na Afrika. Wamegusia fursa za ushirikiano katika elimu, sayansi, TEHAMA, uwekezaji na maeneo mengine ya kimkakati.
Sitanii, miongoni mwa mafanikio makubwa ya ziara hii ni kuimarika kwa diplomasia ya kiuchumi. Tanzania imetumia fursa hii kujitangaza kama kivutio cha uwekezaji kwa wawekezaji wa Urusi katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu, nishati, teknolojia ya nyuklia, gesi asilia, kilimo, madini, urani, utalii, usafiri, viwanda, ubunifu, akili bandia (AI) na maendeleo ya rasilimali watu.

Urusi tayari imeonyesha mwitikio chanya, ikiwa na mradi mkubwa wa uwekezaji wa dola bilioni 1.2, takribani Sh trilioni 3.2, katika mradi wa Urani wa Mto Mkuju mkoani Ruvuma. Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, ambayo ni kampuni tanzu ya ROSATOM, inaongoza mradi huo unaotarajiwa kuzalisha tani 3,000 za urani kwa mwaka, na huenda ukaifanya Tanzania kuwa ya pili kwa uzalishaji wa urani barani Afrika baada ya Msumbiji. Pia unatarajiwa kutoa ajira kwa vijana takribani 20,000.
Sitanii, Rais Samia na Rais Putin pia wamejadili ushirikiano wa uhamishaji wa teknolojia, ikiwemo mpango wa Tanzania kuanza uzalishaji wa umeme wa nyuklia hadi megawati 100 kwa kushirikiana na ROSATOM. Lengo ni kuwa na mtambo wa kwanza wa nyuklia nchini ifikapo mwaka 2029. Nishati ya nyuklia inatoa umeme wa uhakika, wa kiwango kikubwa na usio na hewa ukaa, na inaweza kuleta mapinduzi katika usalama wa nishati na ukuaji wa viwanda nchini.
Nishati hiyo inatoa mbadala wa uhakika wa umeme wa maji ambao huathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Rais Samia amebainisha kuwa hakuna nchi iliyoweza kujenga uchumi wa viwanda na ajira za kutosha kwa watu wake bila nishati ya uhakika na ya kiwango kikubwa.
Urusi imeonyesha utayari wa kusaidia uwekezaji katika gesi asilia, LNG, umeme wa maji na nishati ya uhakika inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Hii inatarajiwa kuongeza ajira na mapato ya taifa. Rais Samia pia alishiriki Jukwaa la Biashara na Uwekezaji la Tanzania–Urusi lililowakutanisha wafanyabiashara wa pande zote mbili kujadili fursa za ushirikiano.
Ushiriki wa Tanzania katika Jukwaa la Kiuchumi la Kimataifa la St. Petersburg (SPIEF) uliipa nchi nafasi ya kujitangaza katika utalii, fursa za uwekezaji na kushiriki katika majadiliano ya uchumi wa dunia. Tanzania imeonyesha mafanikio yake ya mageuzi ya kimfumo, ikiwemo kauli ya Rais Samia kwamba sasa mwekezaji anaweza kusajili kampuni ndani ya saa 24 iwapo ana nyaraka zote zinazotakiwa.

Ziara hiyo pia imefungua milango ya ushirikiano katika elimu ya juu na utafiti wa kisayansi, ambapo taasisi za Tanzania na Urusi zitashirikiana katika mafunzo, utafiti na ubunifu ili kusaidia maendeleo ya viwanda na rasilimali watu. Kwa sasa wanafunzi 150 wa Tanzania wanasomea Urusi, na pande mbili zimekubaliana idadi hiyo iongezwe.
Sitanii, kidiplomasia, ziara hii inaonyesha msimamo wa Tanzania kuendelea na sera ya kutofungamana na upande wowote kwa kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani. Urusi imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Afrika, na Tanzania inaendelea kuimarisha sera yake ya kutofungamana na upande wowote kwa maslahi ya maendeleo.
Rais Samia amesisitiza wazi kuwa Tanzania inavutia uwekezaji kutoka pande zote za dunia. Ameitaja Marekani kama mwekezaji mkubwa katika miradi ya LNG Lindi, nikeli Kabanga Ngara, grafiti Lindi na maeneo mengine. Pia alitaja Umoja wa Ulaya, Japan, China, India, Indonesia, Australia na wengine kuwa na uwekezaji mkubwa nchini.
“Sera yetu ni kutofungamana na upande wowote. Tuko wazi na tunashirikiana na kila mmoja kwa maendeleo ya pamoja na dunia yenye amani,” amesema Rais Samia.

Ziara hiyo pia ina umuhimu wa kijiopolitiki, kwani imefanyika wakati ambapo ushirikiano wa kimataifa unabadilika na mataifa ya Afrika yanatafuta washirika mbalimbali. Tanzania imejipambanua kuwa na sera ya kutofungamana na upande wowote katika ushirikiano wa kimataifa huku ikilinda maslahi yake ya taifa.
Kwa ujumla, ziara ya Rais Samia nchini Urusi imeimarisha diplomasia, kukuza uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa elimu na teknolojia, na kuongeza sauti ya Tanzania katika majukwaa ya kimataifa. Hata hivyo, mafanikio halisi yatapimwa kwa utekelezaji wa makubaliano haya katika ajira, viwanda na maendeleo ya wananchi.
Sitanii, ziara hii imehuisha kwa namna mpya misingi ya Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote (NAM) iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, na imefungua ukurasa mpya katika historia ya diplomasia ya Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania.







Ushauri, maoni 0784 404 827

