Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Ubalozi wa Finland nchini Tanzania, kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania kupitia Mpango wa Ubunifu wa FUNGUO, wameadhimisha Siku ya Misitu ya Finland 2026 yenye kaulimbiu ya “Kufanya Biashara na Finland.”
Tukio hilo limewakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, wajasiriamali na wataalamu wa misitu kutoka Finland na Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kukuza maendeleo endelevu katika sekta ya misitu.
Miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni mijadala kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya misitu nchini Tanzania, mawasilisho kutoka kwa makampuni ya Finland, mikutano ya biashara baina ya wadau na maonyesho ya teknolojia na suluhisho endelevu za misitu kutoka nchi hizo mbili.
Hafla hiyo pia ilishuhudia uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji katika Sekta ya Misitu Tanzania (Tanzania Forest Sector Investment Guide).
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting, amesema ushirikiano wa kibiashara ni nguzo muhimu katika kufungua fursa zilizopo katika sekta ya misitu nchini Tanzania.
“Siku ya Misitu ya Finland inatoa fursa ya kipekee kwa makampuni, wabunifu na wawekezaji kutoka nchi zetu mbili kujenga mahusiano, kubadilishana uzoefu na kubaini maeneo yenye fursa za ushirikiano wa kivitendo,” amesema Theresa.
Ameongeza kuwa tukio hilo linaonesha dhamira ya muda mrefu ya Finland ya kuunga mkono maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini Tanzania kupitia uwekezaji, ubunifu na ushirikiano wa karibu na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Misitu na Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras, amesema sekta ya misitu nchini Tanzania bado ina fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu.
“Finland imekuwa miongoni mwa washirika wetu muhimu katika maendeleo ya sekta hii. Ushirikiano wa moja kwa moja wa kibiashara ndio unaohitajika ili kubadilisha malengo yetu ya pamoja kuwa ajira, ongezeko la thamani na ukuaji endelevu wa uchumi,” amesema.
Taasisi ya Finnpartnership nayo imewasilisha huduma zake kwa washiriki wa Tanzania, hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya za ushirikiano kati ya makampuni ya Finland na Tanzania pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mifumo ya ufadhili wa pamoja kwa ajili ya kukuza biashara na ubia wa kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya Finnfund, Naibu Mtendaji Mkuu, Minnamari Marttila, amesema mikutano ya biashara iliyopangwa vizuri inaweza kuwa chachu ya mageuzi makubwa ya kiuchumi.
“Siku ya Misitu ya Finland inatengeneza mazingira yanayowezesha makampuni kujenga ushirikiano wa muda mrefu kupitia kubadilishana maarifa, uhamishaji wa teknolojia, uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara,” amesema.
Kivutio kikuu cha maadhimisho hayo kilikuwa ni maonyesho ya makampuni yanayofadhiliwa kupitia Mpango wa #GreenCatalyst, unaofadhiliwa na Serikali ya Finland chini ya Mradi wa Ubunifu wa FUNGUO unaotekelezwa na UNDP Tanzania.
Mpango huo unakamilisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa Finland unaojulikana kama FORLAND, wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 61, unaolenga kuimarisha ukuaji endelevu na jumuishi wa sekta ya misitu nchini Tanzania.
Kupitia awamu ya kwanza ya ufadhili wake, #GreenCatalyst umewekeza zaidi ya Sh bilioni moja katika makampuni 14 yanayojihusisha na usimamizi endelevu wa misitu, usindikaji wa mazao ya misitu wenye kuongeza thamani, teknolojia zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na suluhisho za uchumi mzunguko.
Uwekezaji huo unaongeza nguvu katika dhamira ya muda mrefu ya Finland ya kuendeleza sekta ya misitu nchini Tanzania. Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Finland imewekeza euro milioni 45, sawa na takribani Sh bilioni 136.3, katika sekta hiyo kwa lengo la kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu, maendeleo ya ujuzi, ubunifu na ushirikiano wa sekta binafsi.
Akizungumza kwa niaba ya UNDP Tanzania, Meneja wa Mradi wa FUNGUO, Joseph Manirakiza, amesema ubunifu hustawi pale ambapo wajasiriamali wanapata zaidi ya ufadhili pekee.
“Ubunifu unahitaji pia mitandao, masoko na ushirikiano. Siku ya Misitu ya Finland ni jukwaa muhimu linalowawezesha wajasiriamali wetu wa #GreenCatalyst kuunganishwa na wadau mbalimbali na kukuza biashara zao,” amesema.
Naye mwakilishi wa mradi wa FORLAND, Masasa Makwassa, ameipongeza Finland kwa kuandaa maadhimisho hayo na kusisitiza kuwa mradi huo utaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha malengo ya pamoja ya Tanzania na Finland katika sekta ya misitu yanafikiwa.
Amesema ushirikiano huo utaendelea kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za misitu, kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi huku ukihifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.



