Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata
watuhumiwa wanne wanaohusishwa na mauaji ya mfanyabiashara raia wa
China, Fauzani Lee, yaliyotokea hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema hali ya usalama katika jiji hilo inaendelea kuwa shwari huku shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa zikiendelea kama kawaida.

Amesema jukumu kubwa la Jeshi la Polisi ni kuhakikisha wananchi wanafuata sheria na kudumisha amani ya nchi.

“Napenda kuwakumbusha kuwa tarehe 16 Mei, 2026, Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam liliwaarifu wananchi kuwa linaendelea na
uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya mfanyabiashara aliyefahamika kwa
jina la Bhaozan LI mwenye asili ya China aliyekuwa mmiliki wa kiwanda
cha kuchakata chupa kiitwacho XIL LI kilichopo eneo la Mabibo Ubungo
Dar es Salaam ambaye aliuawa kikatili na watu waliodaiwa kuwa ni walinzi wa kiwanda hicho,” amesema .

Amesema mfanyabiashara huyo aliuawa kikatili na watu waliodaiwa kuwa
walinzi wa kiwanda hicho, tukio ambalo lilizua taharuki kubwa miongoni
mwa wananchi na watu waliokuwa wanamfahamu.

Muliro amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi liliahidi kufanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiuchunguzi vilivyopo ndani ya jeshi hilo.

“Baada ya ufuatiliaji wa kina, tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa
wanne katika maeneo tofauti kuhusiana na tukio hili la mauaji,”
amesema .

Alieleza kuwa watuhumiwa hao walipohojiwa kwa kuzingatia taratibu za
kisheria, walikiri kupanga njama kwa pamoja kabla ya kumvamia marehemu
usiku na kumuua baada ya kumuibia kiasi cha shilingi milioni tisa.

“Watuhumiwa hao walidai kuwa fedha hizo zilikuwa ndani ya kiwanda
hicho. Baada ya kutekeleza tukio hilo, walitoroka na kuelekea maeneo
tofauti,” amesema .

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Godson Simon, maarufu kwa jina la
Lazier (25), mkazi wa Hokolili, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro;
Mwingione Elisha Saitoti maarufu kama Luqumai (24), mkazi wa Mkonde,
Handeni mkoani Tanga; Godfrey Laban maarufu kama Moleli (30), mkazi
wa Makongo, Kinondoni; pamoja na Godson Pinel maarufu kama Iisika (24),
mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Muliro amesema baadhi ya watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na tukio
hilo na kueleza kuwa walitumia sehemu ya fedha walizoziiba kununua ng’ombe, ambao wamewaonyesha wachunguzi.

Amesema uchunguzi wa shauri hilo unaendelea kukamilishwa ili
watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazowakabili.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu,
akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma kwa wahalifu na
litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

“Uhalifu mara nyingi huwaingiza wahusika katika migogoro mikubwa ya
kisheria yenye madhara makubwa kwa maisha yao. Tunawashukuru wananchi
waliotupatia ushirikiano mkubwa uliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hawa ambao watafikishwa mahakamani,” amesema.