Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea ujumbe wa wataalamu kutoka Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI) chini ya Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF), wenye lengo la kuimarisha Mtandao wa Vituo vya Hali ya Hewa nchini ili kufikia viwango vya Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi wa Hali ya Hewa (GBON).
Mtandao huu ulioanzishwa na Shirika la Hali ya hHewa Duniani (WMO) ukiwa na malengo ya kuimarisha ukusanyaji wa data za hali ya hewa duniani, Kuhakikisha data za uangazi zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, Kuboresha utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema, Kusaidia nchi hasa zinazoendelea, kutimiza mahitaji ya uangazi wa hali ya hewa yanayowekwa na WMO.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ziara hiyo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema kuwa ujumbe huo wa kitaalamu unaonesha dhamira ya pamoja ya kuendelea kuimarisha uwezo wa TMA katika uangazi wa hali ya hewa na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa kupitia mradi wa SOFF unaleta matokeo chanya na endelevu yanayoiwezesha Tanzania kuendelea kutimiza viwango vya GBON.
“Lengo letu ni kuhakikisha TMA inaendelea kutimiza viwango vya GBON kwa muda mrefu huku ikiboresha ubora na usahihi wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa jamii taifa, kiatika kanda na kimataifa,” alisema Dkt. Chang’a.
Ziara hiyo ya kitaalamu ita tathmini uwezo wa TMA katika maeneo mbalimbali ikiwemo mfumo wa ubadilishanaji wa taaarifa za hali ya hewa kimataifa, matengenezo na ukarabati wa vifaa, mchakato wa kujenga uwezo kwa wataalamu wa TMA, huduma za uhakiki wa vifaa pamoja na uendeshaji wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa vya ardhini na anga la juu.
Nae Meneja wa Mradi kutoka DMI, Dkt. Sebastian Hornum, alisema, “Ziara hii inatoa fursa muhimu ya kufanya kazi kwa karibu na wataalamu wa TMA ili kubaini mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuimarisha uwezo wa kiufundi na kufikia viwango vya kimataifa vya uangazi wa hali ya hewa.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Uratibu wa Mradi wa SOFF (PTCC) kutoka UNDP, Dkt. Abbas Kitogo, alisema:
“Mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yanaakisi ushirikiano mzuri uliopo kati ya TMA, DMI na UNDP. Tutaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kuhakikisha Mradi wa SOFF unatekelezwa kikamilifu kwa faida endelevu za kiuchumi na kijamii nchini.”
Ziara hiyo itahusisha kutembelea vituo vya uangazi wa hali ya hewa vilivyopo Dodoma na Dar es Salaam ambavyo vimejumuishwa katika mtandao wa GBON ili kutathmini hali ya uendeshaji na kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi.


