Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es salaam
Benki ya CRDB, kupitia udhamini wake mkuu wa CRDB Bank Bunge Grand Bonanza 2026, imekabidhi vifaa vya michezo na zawadi mbalimbali zitakazotumika katika bonanza hilo linalotarajiwa kufanyika Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Bonanza hilo litawakutanisha wabunge, watumishi wa Bunge, mabalozi wa nchi mbalimbali pamoja na wadau wengine katika michezo tofauti ikiwemo mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, mpira wa kikapu na michezo mingine ya kijamii.
Akizungumza Leo Jijini Dar es salaam Juni 17,2026 wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa, amesema benki hiyo inajivunia ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wabunge ambao ni miongoni mwa wadau muhimu wa benki hiyo.
Amesema ushirikiano huo haujikita katika huduma za kifedha pekee, bali pia katika shughuli za kijamii na maendeleo ya wananchi kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuinua ustawi wa jamii.
“Ushirikiano wetu hauishii kwenye huduma za fedha pekee bali unaimarishwa zaidi kupitia shughuli za kijamii na maendeleo ya wananchi, ikiwamo utekelezaji wa Programu ya Imbeju inayosimamiwa na CRDB Bank Foundation yenye lengo la kukuza elimu ya fedha, kujenga uchumi jumuishi na kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wananchi,” amesema Mwambapa.
Ameeleza kuwa Bunge Grand Bonanza ni jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano kati ya Bunge, wananchi na taasisi mbalimbali, huku likihamasisha jamii kushiriki mazoezi ya viungo kama njia ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Katika hafla hiyo, Benki ya CRDB imekabidhi vifaa mbalimbali vya michezo vikiwemo jezi za mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu na vifaa vingine vitakavyotumika wakati wa mashindano, sambamba na medali na makombe kwa washindi. Jumla ya udhamini huo una thamani ya Shilingi milioni 450.
Bonanza la mwaka huu linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, huku Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya waandaaji, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa mdhamini mkuu wa tukio hilo ambalo limekuwa sehemu ya ratiba ya kila mwaka ya Bunge kuelekea kuhitimishwa kwa vikao vya Bajeti.
Amesema bonanza hilo limeendelea kuwa daraja la kuwaunganisha viongozi, wananchi na wadau wa maendeleo kupitia michezo, huku akiwahamasisha wakazi wa Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki na kushuhudia mashindano hayo.
“Mchezo una mashabiki, hivyo tunawaalika Watanzania wote kujitokeza kuwashabikia wabunge na viongozi wao huku wakijifunza umuhimu wa afya kupitia michezo,” amesema Sanga.
Aidha, amepongeza mchango wa Benki ya CRDB katika kukuza michezo nchini na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za umma.
“Ushirikiano huu ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi na taasisi za umma zinavyoweza kushirikiana kuhamasisha michezo, kujenga afya njema na kuimarisha umoja miongoni mwa viongozi na wananchi kwa ujumla,” amesema.
Kwa mujibu wa ratiba ya bonanza hilo, shughuli zitaanza kwa matembezi ya pamoja kabla ya kuendelea na michezo ya bao na karata. Baadaye jioni, timu ya wabunge itavaana na mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali nchini katika mchezo wa soka, huku katika mpira wa pete na mpira wa kikapu wabunge wakichuana na wafanyakazi wa Benki ya CRDB.
Sanga amesema kuhusishwa kwa mabalozi katika bonanza hilo kunalenga kuimarisha diplomasia ya michezo na kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine.
“Nimepata fursa ya kushiriki CRDB Bank Marathon nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na nimejionea jinsi michezo inavyounganisha watu bila kujali tofauti zao. Ndiyo maana mwaka huu tumewakaribisha mabalozi ili kupanua wigo wa ushirikiano na kuimarisha diplomasia ya michezo kati ya Tanzania na mataifa mengine,” amesema Sanga.
Bonanza hilo linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo na kijamii yatakayowakutanisha viongozi wa kitaifa, wadau wa maendeleo na wananchi katika mazingira ya kujenga afya, umoja na mshikamano wa kitaifa.









