Na Mwandishi Wetu
WADAU wa mazingira kutoka Taasisi ya Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) ya Ujerumani wameonesha nia ya kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo endelevu ikiwemo uhifadhi wa mazingira, nishati safi, biashara ya kaboni, maendeleo ya vijana na kilimo.
Nia hiyo ilibainishwa katika mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa HRNS, Bw. Olaf Tschimpke, yaliyolenga kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Serikali ya Tanzania.
Kikao hicho kimefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 64 wa Wataalam wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (SB64) unaofanyika Bonn, Ujerumani.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Muyungi aliwasilisha vipaumbele vya Taifa vilivyomo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo maendeleo ya masoko ya kaboni, nishati jadidifu, uchumi wa buluu, nishati safi ya kupikia na ushiriki wa vijana katika uhifadhi wa mazingira.
Aidha, Dkt. Muyungi alieleza umuhimu wa kupata wadau wa kusaidia kuendesha Kituo cha Vijana cha Afrika cha Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi kilichopo Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Bw. Tschimpke alisema HRNS ina uzoefu wa kusaidia wakulima wadogo wa kahawa, kulinda mazingira na kuwawezesha vijana katika nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Tanzania, Uganda na Ethiopia.
Maeneo yaliyotajwa kuwa na fursa za ushirikiano ni pamoja na kusaidia wakulima wadogo wa kahawa, kuanzisha Muungano wa Kudhibiti Uchafuzi wa Plastiki nchini, kuendeleza masoko ya kaboni, uwekezaji katika nishati ya jua, programu za michezo kwa vijana, mafunzo ya mazingira na ujasiriamali kwa vijana pamoja na uwekezaji katika teknolojia za usafiri wa umeme (e-mobility).
Pia, pande hizo mbili zimekubaliana kuendelea na mazungumzo kupitia kikao cha ufuatiliaji kitakachofanyika mwezi Julai mjini Bonn, Ujerumani, pamoja na kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) itakayobainisha maeneo ya ushirikiano na utekelezaji wake.
Vilevile, imekubaliwa kuandaliwa kwa mkutano wa wadau utakaowakutanisha washirika wa HRNS na Serikali ya Tanzania nchini Tanzania ili kujadili kwa kina fursa za ushirikiano, uwekezaji na utekelezaji wa maeneo yaliyobainishwa kuwa na maslahi ya pamoja.
Katika hatua nyingine, Dkt. Muyungi, amekutana na Mwakilishi wa Sekretarieti ya Santiago Network, Bw. Lorenzo Guadagno kwa lengo la Lengo kuu la mazungumzo hayo kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Santiago Network, pamoja na kujadili namna ya kuhakikisha kuwa Ofisi ya Kanda ya Santiago Network kwa Afrika iliyopo Dar es Salaam.
Tanzania, inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan Hasara na Uharibifu (Loss and Damage).
Dkt. Muyungi alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na Santiago Network ili kuhakikisha kuwa ofisi hiyo ya kikanda inakuwa kitovu muhimu cha uratibu, ujenzi wa uwezo, kubadilishana uzoefu na utoaji wa msaada wa kiufundi kwa nchi za Afrika. Alieleza kuwa Tanzania iko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa manufaa ya bara la Afrika.
Kwa upande wake, Bw. Guadagno alieleza dhamira ya Sekretarieti ya Santiago Network ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania na wadau wengine wa kikanda ili kuhakikisha kuwa huduma na msaada wa kiufundi unaotolewa kupitia ofisi ya Dar es Salaam unawafikia walengwa kwa wakati na kwa ufanisi, sambamba na malengo ya Santiago Network ya kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na changamoto za hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Pande zote mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha kuwa Ofisi ya Kanda ya Santiago Network kwa Afrika inakuwa chombo madhubuti cha kusaidia nchi za bara hilo katika kujenga ustahimilivu na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.




