Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es salaam

Raia wanne wa China, Deng Anqing, Fan Zhong Hua, Zhang Jianjun na Deng Qiang, wanaotuhumiwa kumteka nyara mwenzao, wameshindwa kusomewa mashtaka yanayowakabili katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Kinyerezi jijini Dar es Salaam kutokana na kukosekana kwa mkalimani.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Herieth Mwailolo, kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayohusiana na makosa ya uhujumu uchumi. Hata hivyo, zoezi hilo halikuweza kuendelea baada ya kubainika kuwa Mahakama haikuwa na mkalimani wa kuwawezesha kuelewa mwenendo wa shauri.

Ilielezwa mahakamani kuwa washtakiwa hao hawafahamu lugha ya Kiswahili wala Kiingereza, hivyo uwepo wa mkalimani ni muhimu ili kuhakikisha wanapata haki ya kuelewa mashtaka yanayowakabili na taratibu zote za kisheria zinazofanyika mahakamani.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mwailolo aliahirisha kesi namba 13626/2026 hadi kesho, akielekeza hatua zichukuliwe kuhakikisha mkalimani anapatikana ili washtakiwa hao waweze kusomewa rasmi mashtaka yao na shauri kuendelea kwa mujibu wa sheria.

Kesi hiyo inahusisha tuhuma za utekaji nyara wa raia mwenzao wa China, huku uchunguzi na taratibu nyingine za kisheria zikiendelea.