Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam,
SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kuendelea kutumia kalamu na sauti zao kama nyenzo muhimu katika kukuza maadili, uwajibikaji na uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Jaji (Mstaafu), Sivangilwa Mwangesi ambaye ni Kamishna wa Maadili ya Umma, Katibu wa Usimamizi wa Maadili, Kassim Mkwawa katika ufunguzi wa mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari uliofanyika leo Juni 19, 2026 jijini Dar es Salaam.
Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kujenga taifa lenye viongozi waadilifu na jamii inayozingatia misingi ya maadili.
Mkwawa alieleza kuwa kwa miaka minne sasa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa na utamaduni wa kukutana na wahariri kwa lengo la kujenga ushirikiano, kupeana elimu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, pamoja na kujadili namna bora ya kuimarisha maadili nchini.
Alisema ushirikiano kati ya Sekretarieti na vyombo vya habari umeleta matokeo chanya, hasa katika kusaidia taasisi hiyo kupata taarifa zinazohusu changamoto za kimaadili miongoni mwa viongozi wa umma.
“Vyombo vya habari vimekuwa msaada mkubwa sana kwetu. Kupitia habari mnazochapisha, tumekuwa tukipata taarifa zinazotusaidia kutambua changamoto mbalimbali za kimaadili na kuzifanyia kazi,” alisema.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, katika mwaka wa fedha 2025/26, Sekretarieti imefanya ziara katika kanda nane nchini kwa lengo la kukutana na wahariri wa kanda mbalimbali na kujadiliana kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika kukuza maadili ya viongozi wa umma.
Alisisitiza kuwa wahariri na wanahabari ni wadau muhimu kwa sababu wana uwezo wa kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa kwa haraka, huku pia wakiwa na nafasi ya kuishawishi jamii kuelekea katika mwelekeo chanya.
Aidha, aliwataka wahariri kujitafakari na kujiuliza mchango wao binafsi katika kukuza maadili kupitia kazi zao za kila siku.
“Ni muhimu kila mmoja wetu kujiuliza; je, tunachangia vipi kukuza uadilifu nchini? Je, tunasaidiaje kufichua vitendo vya ukiukwaji wa maadili? Hii ni kazi yetu sote,” alisisitiza.
Mkwawa alieleza kuwa taifa lenye viongozi waadilifu hujenga mazingira bora ya maendeleo kwa kuhakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wananchi wote kwa usawa.
Alionya kuwa kukosekana kwa uadilifu kunachochea malalamiko, manung’uniko, upendeleo na mgawanyo usio sawa wa rasilimali za taifa.
Katika wito wake kwa wahariri, aliwahimiza kuendelea kuwa wazalendo na kutumia taaluma yao kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na viongozi waadilifu.
Pia alipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao, jambo ambalo limechangia kudumisha amani na kulinda maadili ya Kitanzania licha ya changamoto za utandawazi.
Kwa ujumla, ujumbe mkuu wa mkutano huo ulikuwa ni kusisitiza kuwa ujenzi wa taifa lenye viongozi waadilifu unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za umma, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, aliwapongeza viongozi wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma kwa mafunzo yaliyotolewa kwani yatawasaidia wahariri katika utendajikazi kwa kuelimisha jamii na kuwa na taifa lenye kufuata misingi ya maadili.
“Haya mafunzo ni nyenzo muhimu kwa wahariri kwani yatasaidia jamii kupata elimu na kuwa wazalendo na taifa lenye umoja, mshikamano na kuwa na viongozi waadilifu” alisema Balile.
Balile alisema kuwa utaratibu wa kuwaelimisha wahariri maadili kwa viongozi wa umma yatachochea kuwa na jamii inayozingatia misingi ya maadili nchini.
















