Na Mwandishi Wetu,JamhurieMdia,
Dar es Salaam
Benki ya CRDB kupitia kitengo chake cha Youth Banking imeendelea kuonesha moyo wa kujali jamii baada ya kuisadia familia ya Bw. Simon Mkwizu iliyojaliwa kupata watoto watano kwa wakati mmoja, kwa kuwafungulia akaunti maalumu za Junior Jumbo na kuweka kiasi cha Sh. milioni 1.5 kwa kila mtoto.
Akizungumza leo Juni 19, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuishika mkono familia hiyo, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile, amesema kuzaliwa kwa watoto hao ni tukio la kipekee na baraka kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Amesema mbali na kuwafungulia watoto hao akaunti zenye jumla ya Sh. milioni 7.5, benki hiyo pia imemfungulia mama yao akaunti ya Malkia yenye amana ya Sh. milioni 2.5 pamoja na akaunti ya akiba yenye Sh. milioni 1.5 kwa ajili ya kumsaidia kuanzisha shughuli za ujasiriamali atakapopata nafuu.
“Zawadi yetu kwa familia hii ni kuwafungulia watoto wote watano akaunti za Junior Jumbo na kuweka Sh. milioni 1.5 kwa kila mmoja. Mama yao pia tumemfungulia akaunti ya Malkia na kuweka Sh. milioni 2.5 pamoja na Sh. milioni 1.5 kwenye akaunti ya akiba. Aidha, watoto wote wataunganishwa kwenye huduma ya bima ya afya,” alisema Mwile.
Aliongeza kuwa benki hiyo imemkabidhi baba wa familia hiyo, Bw. Simon Mkwizu, bajaji ambayo itamsaidia kujiongezea kipato na kukidhi mahitaji ya familia inayokua.
“Kwenye uzao huu wa baraka, sisi CRDB tumekuja kuwashika mkono. Tumeona huu ni muujiza wa Mungu. Pia tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya kupitia uwekezaji katika wahudumu wa afya na vifaa tiba, jambo ambalo limechangia watoto hawa kuzaliwa salama,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, alisema hospitali hiyo imeandika historia kwa mara ya kwanza kupokea watoto watano waliozaliwa kwa wakati mmoja.
“Kwa kawaida tulikuwa tunasikia au kupokea mapacha wanne, lakini hawa watano ni wa kipekee. Tukio hili limegusa Watanzania wengi na sisi kama hospitali tutahakikisha wanaendelea kupata huduma bora hadi watakapokuwa salama kabisa,” alisema Dkt. Kimambo
Alieleza kuwa mmoja wa watoto hao alizaliwa akiwa na uzito wa gramu 800, lakini anaendelea vizuri chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya.
Dkt. Kimambo alisema Hospitali ya Taifa Muhimbili ina wataalamu wabobezi wa watoto wachanga na wenye uzito mdogo, jambo linalowezesha watoto hao kuendelea kupata huduma stahiki.
Alibainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya, hususan katika huduma za mama na mtoto.
Aidha, alikumbusha kuwa Februari 4, 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipokea Tuzo ya Kimataifa ya The Global Goalkeeperbay Gates Foundation kutokana na mafanikio ya Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Kimambo alisema watoto hao bado wanaendelea kupatiwa huduma hospitalini na kwamba wadau mbalimbali wamejitokeza kuwasaidia, huku baadhi wakiahidi kugharamia maziwa yao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Naye baba wa watoto hao, Simon Mkwizu, aliishukuru Benki ya CRDB kwa msaada huo mkubwa na kuahidi kuwa balozi wa kuitangaza benki hiyo kutokana na mchango wake katika kuunga mkono familia yake wakati huu muhimu.
“Tumeguswa sana na msaada huu. Tunawashukuru CRDB na wadau wote waliotusapoti. Ahadi yangu ni kuwa balozi mzuri wa huduma za benki hii kwa jinsi walivyotusimamia katika kipindi hiki,” alisema Mkwizu.






