Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema ufugaji wa kisasa unaojumuisha matumizi ya mashamba ya malisho, mbegu bora za mifugo na teknolojia za kisasa ni suluhisho la kudumu la migogoro ya wakulima na wafugaji inayotokana na ongezeko la matumizi ya ardhi nchini.

Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo wakati akifungua Maonesho ya Tri-Nations Livestock Expo yaliyofanyika Ubena, Chalinze mkoani Pwani, ambapo amewataka wafugaji kubadili mifumo ya ufugaji kwa kuwekeza katika malisho na teknolojia ili kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama hata kwa mifugo michache.

Aidha, Mwigulu amewahimiza wazalishaji kuhakikisha ubora wa bidhaa unakuwa sehemu ya utamaduni wa kila siku badala ya kuandaa bidhaa bora kwa ajili ya maonesho pekee.

Vilevile, Waziri Mkuu amepongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya mifugo na kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa kuondoa zaidi ya kodi na tozo 300 zilizokuwa zikikwamisha ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amefafanua mkoa huo unaendelea kufanya vizuri katika sekta za ufugaji, uvuvi na viwanda, kwani hadi sasa mkoa umeanzisha ranchi ndogo 921 zenye ukubwa wa hekta 38,319 na kutoa hati 419 kwa wafugaji.

Waziri wa Mifugo, Dkt. Bashiru Kakurwa, amesema maonesho hayo yanalenga kuwakutanisha wadau wa sekta ya mifugo ili kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya na kupanua fursa za masoko.