Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pemba

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Anna Athanas Paul, amewataka washiriki wa mafunzo ya utambuzi na uorodheshaji wa vikundi vya uzalishaji kiuchumi vya wanawake kufanya kazi kwa umakini na weledi ili kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana kwa ajili ya utekelezaji wenye mafanikio wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA).

Akifunga rasmi mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika Ukumbi wa Makaonyo , Chake Chake, Pemba, Waziri Anna alisema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa miaka mitano unaolenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake pamoja na kuimarisha huduma za kupinga na kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Mhe. Anna alisema washiriki wamepatiwa ujuzi wa kutumia mfumo wa kidijitali wa Kobo Toolbox katika ukusanyaji wa taarifa za vikundi vya uzalishaji, hatua ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi zitakazotumika kupanga hatua mbalimbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi.

“Mafanikio ya zoezi hili ni moja ya nguzo muhimu katika utekelezaji wa mradi huu. Kila dodoso mtakalojaza linabeba mustakabali wa juhudi za Serikali na Wadau wa Maendeleo katika kumkomboa mwanamke na jamii kwa ujumla,” alisema Waziri huyo.

Alieleza kuwa taarifa zitakazokusanywa zitasaidia kubainisha hali halisi ya vikundi vya wanawake, uwezo wao wa uzalishaji, changamoto zinazowakabili pamoja na fursa zilizopo katika masoko na minyororo ya thamani. Aidha, matokeo ya zoezi hilo yatasaidia kupanga mafunzo, ushauri wa biashara na utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vitakavyokidhi vigezo vilivyowekwa.

Kwa mujibu wa Waziri Anna, mradi wa PAMOJA unatekelezwa katika wilaya nne za Unguja na wilaya zote nne za Pemba, ukiwa na lengo la kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za maendeleo.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni daraja muhimu la kuwafikisha wanawake kwenye fursa za kifedha, masoko mapya na maarifa ya biashara yatakayoinua hali zao za maisha, familia zao na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Waziri huyo pia alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendana na malengo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (2025–2030) pamoja na dhamira ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Aliwahimiza washiriki kushirikiana kwa karibu na viongozi wa shehia pamoja na wananchi ili kuhakikisha zoezi la utambuzi na uorodheshaji wa vikundi linafanyika kwa ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Katika hotuba yake, Waziri Anna aliwashukuru wafadhili wa mradi huo, Benki ya Dunia, kwa mchango wao katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mradi huo, pamoja na watendaji na waandaaji wa mafunzo kwa usimamizi mzuri uliofanikisha mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yalianza Unguja kwa Maafisa Wilaya zinatekeleza Mradi na Baadae kufanyika Pemba na Kaulimbiu: “Pamoja kwa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi.”