Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Handeni
SEKTA ndogo ya madini kinywe (graphite) imezidi kuimarika kufuatia ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua na kusindika madini hayo katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Juni 19, mwaka huu, Mwenge wa Uhuru wenye kaulimbiu inayosema “Tanzania ni yetu tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo”, uliweka jiwe la msingi kwenye mradi huo ambao ujenzi wake unagharimu Shilingi bilioni tatu, uliopo kijiji cha Suwa wilayani humo.
Taarifa ya Mkurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya ACE Graphite Tanzania Limited, Vishal Poddar kwa Mwenge wa Uhuru jana Juni 19, 2026, ilieleza kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) Septemba, 2025 ina uwezo wa kusindika tani 12,000 za madini hayo kwa mwaka.
Hivyo, amesema mradi huo ni muhimu katika maendeleo ya sekta ya madini na viwanda nchini, kupitia shughuli za uongezaji thamani kabla ya kuuzwa ndani na kimataifa.
Poddar amesema, ujenzi wa kiwanda hicho ulioanza mwaka 2025 unakadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 3, na utakamilika Desemba, 2026.
Amesema uamuzi wa kuwekeza katika eneo hilo, umetokana na kuwepo kwa mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji, yaliyowawezesha kupata eneo, hati na vibali muhimu vya uwekezaji.
Poddar amesema, kiwanda hicho kimejengwa kwa ajili ya usindikaji wa madini kinywe kwa teknolojia na mashine za kisasa, zinazowezesha uchakataji wa madini katika madaraja mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la kimataifa.
Kwa mujibu wa Poddar, malighafi zinazotumika kiwandani humo zinatoka kwenye kampuni za uchimbaji wa madini kinywe ikiwemo God Mwanga Gems Co. Ltd ya Kwamsisi, Handeni na Synergy Co. Ltd ya Morogoro.
Amesema, pamoja na kuongeza thamani na fedha za kigeni, kiwanda hicho kitatoa ajira 40 za moja kwa moja na zaidi ya watu 50 kwa zisizokuwa za moja kwa moja.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amesema uwekezaji huo ni miongoni mwa viashiria vya mazingira salama kwa wawekezaji yaliyowekwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwang’onda amesema, madini hayo yana soko kubwa ndani na nje ya nchi, kutokana na matumizi yake kwa bidhaa mbalimbali zikiwemo betri za magari na penseli.
Amesema ufanisi wa kiwanda hicho unaotegemea zaidi uhakika wa amani, umoja na mshikamano uliopo nchini, utachangia kuongeza ajira hasa kwa vijana, kuleta maendeleo na ustawi kwa wananchi.





