Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Juma Ramadhan (21), tuhuma za kumuua baba yake mzazi Ramadhan Muna (47) na kumfukia ndani ya chumba chake alipokuwa akiishi maeneo ya Mbezi Kwembe.

Kamanda Jumanne Muliro wa kanda hiyo amesema hayo leo Juni 23, 2026 kuwa mtuhumiwa huyo alitoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Gogoni kilichopo Kimara akidai kuwa baba yake mzazi amepotea.

Baada ya kutoa taarifa hiyo iligundulika aliyepotea ameuliwa na kufukiwa kwenye chumba chake.

“Tulibaini aliyefanya tukio hilo ni mtoto wa marehemu ambaye alitoa taarifa kuwa baba yake Ramadhani amepotea lakini walipohojiwa alieleza jinsi alivyofanya tukio na kumfukia ndani ya chumba cha marehemu tunaendelea na upelelezi,”amesema.

Kwa upande mwingine amesema hali ya usalama katika Mkoa wa Dar es salaam ni salama.

Aidha Kamanda Murilo amewashukuru, wanannchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ushirikiano wao na Jeshi Polisi.