Na Dk Reuben Lumbagala
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni chombo muhimu nchini katika kuhakikisha mipango na mikakati ya maendeleo inatimizwa kikamilifu. Hii inatokana na ukweli kuwa mipango mingi ya maendeleo kama uboreshaji wa sekta za elimu, afya, maji, masoko, viwanda, umeme, barabara, makazi, biashara, inategemea upatikanaji wa raslimalifedha ili ziwezeshe utekelezaji wake.
TRA ina wajibu wa kukusanya kodi kutoka kwa walipakodi wake kama wafanyabiashara, wawekezaji, wafanyakazi na wajasiriamali mbalimbali. Mafanikio ya ukusanyaji kodi, ndiyo msingi wa kuiwezesha serikali kutimiza mipango yake ya maendeleo kwa ustawi na maendeleo ya wananchi.
Sasa TRA imetimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake. TRA imepata mafanikio makubwa sana hasa katika uongozi wa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Rais Dk. Samia aliweka msingi wa serikali yake mapema kwa kuiagiza TRA iwajibike ipasavyo katika kukusanya mapato, lakini mapato hayo yasiwe ya dhuluma. Rais Dk. Samia anataka kila mwananchi mwenye sifa za kulipa kodi alipe.
Aprili 6, 2021, Rais Dk. Samia alipokuwa akiwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao, alitoa maelekezo mahsusi kwa TRA. “Kukusanya kodi kwa mabavu havisaidii kwa muda mrefu. Nimepewa takwimu ya zile taskforce (vikosikazi vya kukusanya kodi) mlizoziunda lakini havisaidii, mnawatisha watu wanalazimika kufunga biashara.”
“Tunazitaka kodi lakini kodi za dhuluma hapana. Kwa sababu hazitatufikisha mbali. Jinsi ya kurudisha wafanyabiashara, kutengeneza wigo wa kukusanya kodi, nafahamu uamuzi huu niliochukua tutayumba kwa miezi miwili, mitatu lakini baada ya muda tutarudi vizuri,” amesema Rais Dk. Samia.
Msisitizo wa kuongeza mapato ulitokana na ukweli kuwa mipango mingi na mizuri aliyonayo Rais Dk. Samia kwa wananchi wake, haitaweza kufanikiwa kama TRA haitakusanya kodi kikamilifu ambayo ndiyo kichochea cha kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Awali, TRA ilikuwa na utaratibu wa kufunga biashara na shughuli mbalimbali pale ambapo mlipakodi atashindwa kulipa kodi kwa wakati.
Vilevile, katika makadirio ya kodi, baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakilalamikia kuwekewa makadirio makubwa tofauti na kiwango cha biashara zao. Hii iliweka uadui mkubwa kati ya TRA na walipakodi nchini.
MAGEUZI MAKUBWA YAMEONDOA UADUI KATI YA TRA NA WALIPAKODI
Kutokana na maelekezo ya Rais. Dk. Samia kwa TRA, uadui uliokuwepo awali kati ya TRA na walipakodi umeondoka. Hii inatokana na mtazamo chanya alioujenga Rais Dk. Samia kwa pande zote mbili.
Kimsingi, pande zote mbili zinategemeana. TRA anamtegemea mlipakodi kwani pindi kodi inapolipwa ndipo inawezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inamnufaisha mlipakodi moja kwa moj.
Rais Dk. Samia akasisitiza pawepo na meza ya mazungumzo na makubaliano ya namna gani mlipakodi atalipa kodi pale ambapo atashindwa kulipa kwa wakati.
Aidha, Rais Samia akasisitiza kuwa kufunga biashara ni kummaliza kabisa mlipakodi kwani biashara yake itakapofungwa, ndipo atashindwa kabisa kulipa kodi kwani hatakuwa na shughuli ya kumuingizia kipato cha kuwezesha kulipa kodi na wala TRA haitaweza kupata kodi yake.
Kongole kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, pamoja na wasaidizi wake nchi nzima wamefanyia kazi maelekezo ya Rais, na sasa tunashuhudia mafanikio ya kumalizika kwa uadui uliokuwepo awali.
Ni faraja kuona tunapoadhimisha miaka 30 ya TRA, kumejengeka uhusiano mzuri kati ya mlipakodi na mamlaka. Hakuna mabavu wala ubabe. Uhusiano mzuri uliopo umewezesha kuongezeka kwa mapato ya serikali.
Mathalani, mwezi Machi, 2026, TRA wamefanikiwa kukusanya trilioni 3.58, na kimsingi, ongezeko la makusanyo yamewezesha hata bajeti ya mwaka 2026/2027, kutegemea mapato ya ndani kwa asilimia 74.2.
Maoni : 0620 800 462




