Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma
Wakati Dunia ikiendelea kutafuta vyanzo vya nishati safi na rafiki kwa mazingira, Tanzania imeendelea kunufaika na hazina kubwa ya gesi asilia inayochochea uzalishaji wa umeme, ukuaji wa viwanda na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Rasilimali hiyo sasa imeendelea kuwa nguzo muhimu ya mkakati wa nchi katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuongeza fursa za uwekezaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema gesi asilia imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Tanzania huku matumizi yake yakiongezeka kutokana na mabadiliko ya teknolojia na juhudi za kimataifa za kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira.
Akizungumza Juni 23, 2026 Wakati wa kuhitimisha maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, Mhandisi Sangweni alisema PURA imeendelea kusimamia kwa karibu shughuli za utafutaji, uchimbaji na maendeleo ya rasilimali za mafuta na gesi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya nchi.
Ameeleza kuwa licha ya Tanzania kuanza shughuli za utafutaji wa mafuta tangu miaka ya 1950 na kuchimba visima zaidi ya 97, bado haijapata mafuta ya kibiashara.
Pia ameeleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana kupitia ugunduzi wa gesi asilia ambayo kwa sasa inatumika katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma.
“Gesi asilia ni hazina muhimu ya taifa inayochangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sekta ya nishati na uchumi wa nchi,” amesema Mhandisi Sangweni.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayoongeza mahitaji ya gesi asilia na kufungua fursa mpya za uwekezaji pamoja na ajira kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Sangweni, PURA imeendelea kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za petroli kupitia ajira, utoaji wa huduma na bidhaa pamoja na ushiriki wa wazawa katika miradi mbalimbali chini ya sera ya ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content).
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo imeanzisha mifumo inayowaunganisha wataalamu wa Kitanzania na wawekezaji ili kuongeza ajira, kuimarisha ujuzi na kuwezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli za sekta ya mafuta na gesi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Eyasi-Wembere pamoja na vitalu vya Lindi na Mtwara vinavyotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumzia hali ya soko la mafuta duniani, Sangweni alisema Tanzania imeendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta licha ya changamoto zinazotokana na migogoro ya kimataifa inayojitokeza katika baadhi ya maeneo duniani.
Amesema nchi za Afrika Mashariki na Kati zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika matumizi na usambazaji wa rasilimali za nishati ili kuhakikisha usalama wa nishati kwa wananchi hata wakati wa misukosuko ya kimataifa.
Sangweni amesisitiza kuwa Afrika inapaswa kuendelea kutumia rasilimali zake za mafuta, gesi na madini kama chachu ya maendeleo ya wananchi wake, huku ikizingatia misingi ya utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu.



