Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Zaidi ya tani 49,000 za mbolea tayari zimesambazwa kwa wakulima nchini kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa mahitaji ya pembejeo za kilimo wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Hata hivyo, pamoja na ongezeko hilo la matumizi ya mbolea, utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi umeendelea kuwa moja ya changamoto zinazotafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Katika kukabiliana na hali hiyo, TFC imeanza maandalizi ya uzinduzi wa kiwanda kipya cha kisasa cha mbolea mkoani Tanga kitakachozalisha mbolea maalum kulingana na mahitaji ya rutuba ya udongo wa maeneo mbalimbali nchini, hatua inayotarajiwa kupunguza utegemezi wa mbolea za nje na kuongeza tija kwa wakulima.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma Juni 23, 2026, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TFC, Nuru Mhando, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha upatikanaji wa mbolea bora nchini.
Amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea zinazolengwa moja kwa moja kulingana na mahitaji ya udongo wa maeneo husika badala ya kutumia mfumo wa mbolea zinazofanana kwa maeneo yote.
“Mradi huu unaotarajiwa kutekelezwa mkoani Tanga ni hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya pembejeo za kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata mbolea inayokidhi mahitaji halisi ya mashamba yao,” amesema.
Mhando amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa ya upimaji wa udongo yatawezesha kubaini kiwango cha virutubisho kilichopo katika mashamba na hivyo kurahisisha utengenezaji wa mbolea inayokidhi mahitaji ya eneo husika.
Amefafanua kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya mbolea, kupunguza gharama kwa wakulima na kuongeza mavuno kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Kiwanda hiki kitazalisha mbolea kulingana na mahitaji ya udongo wa maeneo tofauti nchini. Hii itasaidia wakulima kupata mbolea sahihi na kuongeza mavuno kwa gharama nafuu,” amesema.
Mbali na kuongeza uzalishaji wa mazao, amesema kiwanda hicho kitachangia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi na kusaidia upatikanaji wa pembejeo hizo kwa wakati katika misimu ya kilimo.
Amesema TFC inaendelea kutekeleza jukumu lake la kusambaza mbolea kwa wakulima kupitia mfumo wa ruzuku ambapo Serikali huchangia sehemu ya gharama ili kuwawezesha wakulima kupata pembejeo kwa bei nafuu.
Kwa mujibu wa Mhando, zaidi ya tani 49,000 za mbolea za kupandia na kukuzia mazao tayari zimesambazwa kwa wakulima nchini, huku kampuni hiyo ikiendelea kuhudumia pia wakulima wa tumbaku ambao ni sehemu ya sekta muhimu za uzalishaji wa mazao ya biashara.
Aidha, amesema TFC imeendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo ili kuongeza tija na kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya kilimo unaendelea kuleta matokeo chanya.
Amesisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo katika kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula pamoja na ukuaji wa uchumi wa taifa.



