Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani imeongeza makusanyo ya mapato kutoka Sh bilioni 27 mwaka 2015/2016 hadi Sh bilioni 266 mwaka 2025/2026, sawa na asilimia 113 mafanikio yanayoakisi kuimarisha shughuli za kiuchumi huku ikiendelea kukabiliana na changamoto za magendo na matumizi ya stempu feki.

Akizungumza katika kongamano la wadau na walipa kodi kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake, Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Peter Eliona, alisema ongezeko hilo limetokana na walipa kodi pamoja na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji mapato.

Alisema mwaka 2015/2016 TRA Pwani iliweka lengo la kukusanya Sh bilioni 23 na kufanikiwa kukusanya Sh bilioni 27, huku mwaka 2025/2026 ikiwa na lengo la Sh bilioni 235 na kuvuka hadi Sh bilioni 266.

Eliona alisema mapato hayo yamekuwa chachu ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta mbalimbali.

Hata hivyo, alibainisha kuwa TRA inaendelea kukabiliana na wafanyabiashara wanaojihusisha na magendo, hususan ya spirit na vileo, wanaotumia stempu feki kwa lengo la kukwepa kodi na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Alisema pia mamlaka hiyo inakabiliana na mabadiliko ya teknolojia yanayochochea biashara kufanyika kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali, ili kuhakikisha shughuli hizo zinazingatia ulipaji wa kodi stahiki.

Aliwasihi wafanyabiashara kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka adhabu, penati na usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na kuchelewesha malipo.

Kwa upande mwingine, Eliona alisema TRA imeendelea kuboresha mifumo ya kielektroniki, hatua ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma kwa walipa kodi na kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Pwani, Said Mfinanga, alipongeza mageuzi yanayofanywa na TRA, akisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yamepunguza muda na gharama za wafanyabiashara kupata huduma za kodi.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdallah Ndauka, aliitaka TRA kuendelea kushirikiana kwa karibu na wafanyabiashara kwa kutoa elimu ya kodi na kuwawezesha kukuza biashara zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Pwani, Philemon Maliga, aliomba kuongezwa kwa elimu ya mlipa kodi kwa kundi hilo ili kuongeza uelewa na ushirikiano kati yao na TRA.

Mwenyekiti wa Chama cha Maofisa Usafirishaji Kibaha, Saleh Jamal, alisema madereva wa bodaboda wana mchango mkubwa katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi, akibainisha kuwa idadi yao imefikia 7,700 na wanahitaji kuendelea kupewa elimu ya kodi.

TRA ilianzishwa kwa Sheria Na.11 ya mwaka 1995 na kuanza rasmi shughuli zake za ukusanyaji mapato Julai 1, 1996, ikiwa na jukumu la kusimamia na kukusanya kodi pamoja na mapato mengine ya Serikali Kuu.