Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkutano wa kimataifa wa magonjwa yasiyo ambukiza umezinduliwa leo Juni 23, 2026 katika kituo cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kwa siku tatu ukihusisha watu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Afrika kusini, somalia,kenya na Uganda
Akizungumza katika uzinduzi wa mkutano huo Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema kuwa Afrika inahitaji kuwa na ushirikiano na mshikamano ili kudhibiti na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza.
Mchengerwa amesema watoto na vijana wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo ya vijijini wanawakilisha hali halisi inayotukabili.
Huduma zinazohitajika ili kuwawezesha kuendelea kuishi mara nyingi huwa mbali na hazipatikani kwa urahisi.
“Mara nyingi hakuna mifumo madhubuti ya kuwahudumia, hakuna wahudumu wa afya waliofunzwa vya kutosha, huduma za uchunguzi, dawa, wala ufuatiliaji wa mara kwa mara. Huduma hizi huwa mbali na makazi yao na hivyo kushindwa kuzifikia,”anasema
Katika eneo ninalolizingatia la ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza mtoto anayegundulika kuwa na ugonjwa huo katika maeneo ya vijijini ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara anaweza kuwa na matarajio ya kuishi kwa muda mfupi zaidi kwa takribani miaka 40 ikilinganishwa na mtu aliyezaliwa katika sehemu nyingine ya dunia akiwa na hali hiyo hiyo.
Miaka 12 iliyopita, shirika la Humpty lilianza kusaidia viongozi wa ndani na washirika wa kimataifa waliokuwa na imani kwamba kuunganisha na kuimarisha huduma za kisukari aina ya kwanza pamoja na magonjwa mengine makubwa yasiyoambukiza ilikuwa jambo linalowezekana na muhimu ili kuokoa maisha ya watu.
“Leo tunashuhudia matokeo makubwa ya juhudi hizo na takribani nchi 20 zimeanza kutekeleza au ziko katika hatua za kuanzisha programu za PEN-PLUS huku hospitali zaidi ya 60 sasa zinatoa huduma kwa zaidi ya watu 15,000 wenye magonjwa makubwa yasiyoambukiza na jumla watu zaidi ya 170,000 wakipata huduma kila mwaka katika vituo hivyo,”
Tumeona maendeleo makubwa katika nchi nyingi zilizoanza mapema. Rwanda imefanikiwa kufikia huduma hizo kitaifa. Ethiopia ilizindua mkakati wake wa kitaifa mapema mwaka huu na imejitolea kugharamia asilimia 40 ya gharama kupitia bajeti ya ndani ya taifa.
Katika baadhi ya nchi kubwa zaidi barani Afrika, idadi ya wagonjwa wanaojiandikisha kupata huduma imeongezeka kwa asilimia 117 ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitatu. Kasi ya maendeleo inaendelea kuongezeka.
Hii inaonyesha wazi kwamba mifumo inayoongozwa na nchi zenyewe inaleta matokeo. Serikali zinapoongoza na washirika wanapowekeza katika wahudumu wa afya wa ngazi za wilaya na kuunganisha huduma hizo katika mifumo ya kitaifa badala ya miradi ya muda mfupi, matokeo yake huendelea kuongezeka kwa muda mrefu.
Maendeleo haya ni ushahidi wa kujitolea kwa maafisa wa wizara, viongozi waliopo katika ukumbi huu, pamoja na washirika kama Shirika la Afya Duniani (WHO), mtandao wa PCI Family na taasisi nyingine nyingi zinazotoa msaada wa kitaalamu na kiutekelezaji.
Aidha tunawashukuru wafadhili mbalimbali kama vile Unitaid, Breakthrough T1D, St. Jude, Serikali ya Scotland, Helmsley Charitable Trust na Buffett Foundation ambao wameungana kuunga mkono mageuzi haya ya kitaifa katika sekta ya afya.
Maendeleo haya yana umuhimu mkubwa zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia karibu asilimia 37 ya vifo katika ukanda wa Afrika, na mzigo huo unaendelea kuongezeka. Serikali, washirika na wafadhili wanapaswa kuchukua hatua, lakini namna wanavyochukua hatua ni muhimu sawa na hatua yenyewe.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi amesema magonjwa yasiyoambukiza kwa sasa yanachangia asilimia 37 ya vifo vyote vinavyotokea barani Afrika, yakiongezeka kutoka asilimia 24 mwaka 2000.
Profesa Janabi amesema hayo katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Mkakati wa Kikanda wa PEN-Plus (ICPPA 2026) uliozinduliwa leo katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema mkakati wa PEN-Plus ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo, kwani unalenga kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa magonjwa sugu kama kisukari, seli mundu na magonjwa ya moyo, hususan kwa kuhakikisha wanapata huduma karibu bila kusafiri umbali mrefu.
Aidha amesema mpango huo kwa sasa unatekelezwa katika nchi 20 na umesaidia kuokoa maisha ya zaidi ya watu laki moja, huku nchi kama Rwanda, Malawi na Ghana zikionyesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wake.
Profesa Janabi amesema kuwa PEN-Plus si mradi wa majaribio bali ni ushahidi kuwa usawa wa upatikanaji wa huduma za afya barani Afrika unawezekana.




