Na. Asia Singano, WF- TCHAD
Serikali ya Tanzania imedhamiria kuhakikisha kuwa Wananchi wa Tanzania wanapata huduma za msingi za maji safi na salama kwakuwa maji ni kichocheo muhimu cha mabadiliko ya uchumi na ni muhimu kwa ufanisi wa kilimo, viwanda, uzalishaji wa nishati, maendeleo ya miji, afya ya umma, na ustahimilivu wa tabianchi.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati wa Jukwaa la Maji barani Afrika lenye kaulimbiu, (African Water Forum; from vision to action), linaloendelea kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Radisson mjini N’Djamena, nchini Tchad, alipoongoza Ujumbe wa Tanzania, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).
Alisema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo utekelezaji wake ulianza tarehe 1 Julai 2026 pamoja na Mpango wa Maji wa Rais, wa Maji na Usafi wa Mazingira (Presidential WASH Compact) unaotarajia kuzinduliwa hivi karibuni, Serikali inalenga kuwaleta pamoja taasisi mbalimbali za Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na jamii kupanua upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira, na kukuza uvumbuzi wa kidijitali katika sekta ya maji.
‘’Tumejizatiti kuhakikisha kila kijiji nchini kinapata huduma za msingi za maji safi kufikia mwaka 2031. Hivyo basi, tunasonga mbele na mpango wa uwekezaji wa kimaendeleo utakaounganisha maji kati ya maeneo yasiyo na maji na yale yasiyotoshelezwa” alisema Mhe. Luswetula (Mb).
Alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi huku akizisihi sekta hizo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
‘’Naomba nitoe mwaliko kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kubadilisha sekta yetu ya maji, fursa kubwa zipo katika uwekezaji wa kimkakati kama vile Gridi ya Taifa ya Maji, huduma za WASH zenye kustahimili mabadiliko ya tabianchi, mifumo ya umwagiliaji, matumizi ya kidijitali kwenye sekta ya maji, na utunzaji wa vyanzo vya maji’’ alisema Mhe. Luswetula (Mb).
Alieleza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha mazingira yanayowezesha kuvutia uwekezaji wa muda mrefu, kuweka taratibu za uwazi, sera zinazoweza kutabirika, utawala bora, ili kuyafikia malengo yaliyowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maji, Benki ya Dunia (WB), Afrika, Bw. Saroj Kumar, aliipongeza Tanzania kwa kuwa na mikakati bora ya kuboresha maisha ya wananchi, kuandaa na kuanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imeipa sekta binafsi nafasi ya kuchangia asilimia 70 katika maendeleo ya nchi.
Aliongeza kuwa Benki ya Dunia (WB), inatambua juhudi za Tanzania katika kuendelea kuboresha maisha ya wananchi ambapo juhudi hizo zimejidhihirisha katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 huku Benki hiyo ikiahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa Dira hiyo.





