Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Shinikizo la wito wa kuachiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, linazidi kuongezeka na kuibua mitazamo tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo wa ndani ya nchi na kimataifa.
Mitazamo hiyo inaibuka wakati CHADEMA kupitia vikao vyake vya Kamati Kuu vilivyofanyika mkoani Kigoma hivi karibuni imeazimia pamoja na mambo mengine kufanya operesheni na mikutano ya hadhara katika Kanda za Pwani, Unguja, Pemba na mikoa yote hapa nchini kwa lengo la kushinikiza Lissu aachiwe.
Kwa sasa Lissu anakabiliwa na kosa la uhaini chini ya Kifungu cha 39 (2) (d) kutokana na kauli yake aliyoitoa ya kutaka kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 usifanyike na kesi yake inasikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasisitiza kwamba kesi hiyo ni suala la kulinda haki za binadamu, uhuru wa kisiasa na utawala wa sheria, huku wengine wanaamini kuwa mchakato wa haki unapaswa kuachiwa mahakama bila kuathiriwa na mashinikizo ya kisiasa au kimataifa.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, amesema kuna haja ya kuangalia upya sababu za kuendelea kumshikilia Lissu mahabusu, huku akieleza kwamba mazingira yaliyopo yanaibua maswali kuhusu msingi wa mashtaka yanayomkabili.
“Kauli zinazohusu uchaguzi au ukosoaji wa mfumo wa kisiasa haziwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ni kosa la uhaini, bali suala hilo linaonekana kuwa na sura ya kisiasa kuliko ya kisheria,” amesema.
Pia amesema kama taifa linakusudia kujenga maridhiano na kurejesha mshikamano wa Watanzania, ni muhimu kuachana na misuguano ya kisiasa na kutoa nafasi ya mazungumzo na kuwaachia huru watu wanaoshikiliwa kwa tuhuma zinazohusishwa na siasa, na hatua hiyo itakuwa mwanzo mzuri wa kujenga umoja wa kitaifa.
Amesema historia ya Lissu ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017 imeifanya jumuiya ya kimataifa kuendelea kuwa na wasiwasi kuhusu usalama na haki zake, na kitendo hicho kinaongeza wito wa kuhakikisha anapata haki kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu taswira ya nchi katika masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria, amesema kuna haja ya kuimarisha misingi hiyo ili kulinda sifa ya nchi kimataifa.
Amesema kuna baadhi ya wadau wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kuhusu mwenendo wa mashauri yenye sura ya kisiasa na matumizi ya sheria katika mazingira hayo.
“Hatua za maridhiano na mazungumzo ya kisiasa zinaweza kusaidia kupunguza mpasuko uliopo na kujenga mazingira ya amani, umoja na ushirikiano miongoni mwa Watanzania.
“Wito wa kumuachia Lissu haupaswi kutazamwa kama msimamo wa kisiasa pekee, bali kama fursa ya kuimarisha utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na kujenga taifa lenye mshikamano na maridhiano,” amesema.
Mchambuzi wa Sayansi ya Siasa, Manase Joel, amesema shinikizo kutoka kwa wadau wa ndani na wa kimataifa lina uzito wa kisiasa na kidiplomasia, kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya jumuiya mbalimbali za kimataifa zinazofuatilia masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia.
Amesema serikali inapokabiliwa na wito wa aina hiyo mara nyingi hulazimika kutoa ufafanuzi wa hatua zake ili kulinda taswira ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa, huku ikiendelea kuzingatia sheria za nchi.
Hata hivyo, amesema mjadala wa Lissu kuachiwa au kutoachiwa unapaswa kuongozwa na misingi ya sheria badala ya shinikizo la kisiasa.
“Iwapo kuna kesi mahakamani, mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kuamua kwa kuzingatia ushahidi na sheria. Shinikizo la kisiasa, hata likitoka ndani au nje ya nchi, halipaswi kuingilia uhuru wa mahakama,” amesema.
Kwa upande wake, mdau wa siasa kutoka Dodoma, Hamis Chacha, amesema kauli zinazotolewa na Jumuiya ya Madola pamoja na wadau wengine wa kimataifa zinaonyesha kuwa jamii ya kimataifa inaendelea kufuatilia mwenendo wa demokrasia hapa nchini.
Amesema hali hiyo inaweza kuathiri namna wawekezaji, washirika wa maendeleo na taasisi za kimataifa wanavyoitazama Tanzania, ingawa athari zake hutegemea jinsi serikali itakavyojibu hoja hizo na kuonyesha taasisi zake zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
“Si kila shinikizo la kimataifa linapaswa kuamua mwenendo wa nchi, Tanzania ina Katiba, sheria na taasisi zake. Wapo wanaoona baadhi ya kauli zinazotolewa kuhusu Lissu zina sura ya kisiasa zaidi kuliko ya kisheria. Kwa mtazamo huo, kesi zinapaswa kuendelea mahakamani bila kushinikizwa na makundi ya kisiasa au ya nje,” amesema.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Gaya Sanga, amesema shinikizo linalotolewa na wadau wa ndani na nje ya nchi linaonyesha kuwa suala la Lissu limevuka mipaka ya kesi ya kawaida na sasa linatazamwa kama kipimo cha hali ya demokrasia nchini.
Amesema wadau wa kimataifa wanataka kuona taasisi za haki zikifanya kazi kwa uwazi na kwa kuzingatia haki za msingi.
“Wanaamini serikali ikitoa maelezo ya wazi na kuruhusu mchakato wa haki uonekane kuwa huru, inaweza kuimarisha taswira ya Tanzania badala ya kuidhoofisha,” amesema.
Kwa upande wake, Mhina Nanaukwa, amesema iwapo kuna kesi mahakamani, ni mahakama pekee inayopaswa kuamua kwa kuzingatia ushahidi na sheria na si kwa misingi ya shinikizo la kisiasa.
“Wapo pia wanaochukua msimamo wa kati wakisema pande zote zina hoja, wanaotaka Lissu aachiwe wanasisitiza haki za kisiasa na uhuru wa kushiriki katika siasa.
“Huku wanaopinga wakisisitiza kuwa sheria lazima iheshimiwe bila kujali nafasi ya mtuhumiwa. Wengine wanaona kuwa suala hilo haliwezi kutenganishwa na siasa,” amesema.
Naye Mama Joyce Chiwaligo amesema upinzani unatumika kuhamasisha wafuasi wake na kuonyesha kuna changamoto katika mazingira ya kisiasa, wakati serikali inalenga kuonyesha hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Katibu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO), Bonaventura Mwalongo, amesema shinikizo la kuachiwa Lissu lina uzito wa kisiasa na kidiplomasia, kwa sababu linagusa misingi ya utawala wa sheria, haki za binadamu na taswira ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo, amesema uzito huo haupaswi kutafsiriwa kama ni mamlaka ya kuamuru mahakama au serikali ichukue hatua fulani nje ya utaratibu wa kisheria.
“Kwa mtazamo wangu, wito wa kutaka Lissu aachiwe unaweza kueleweka kwa namna mbili. Kwa upande mmoja, ni utetezi wa haki za kikatiba, haki ya kusikilizwa kwa haki, na umuhimu wa kuhakikisha mchakato wa sheria unazingatia misingi ya haki na usawa.
Kwa upande mwingine, ni sehemu ya mjadala mpana wa kisiasa unaohusisha ushindani wa vyama, mazingira ya uchaguzi na mustakabali wa demokrasia nchini,” amesema.
Kuhusu nafasi ya Rais Samia, amesema Katiba inaweka wazi misingi ya utenganisho wa madaraka na haipaswi kuingilia uamuzi wa mahakama katika kesi inayoendelea.
“Wajibu wake ni kuhakikisha taasisi zote za dola zinafanya kazi kwa uhuru, weledi na kwa kuzingatia sheria, akilinda amani, umoja wa taifa na imani ya wananchi katika mfumo wa haki. Endapo suala linaendelea kuibua mvutano mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia, hekima ya uongozi huonekana katika kuimarisha mazungumzo.
“Kuheshimu sheria, kuhakikisha kesi zinasikilizwa kwa haki na bila ucheleweshaji usio wa lazima na kujenga mazingira yatakayowafanya wananchi wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa wanaamini kuwa haki inatendeka,” amesema.

Chatanda amvaa Tibaijuka
Baada ya Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kusema anaendelea kumshauri Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhati kwamba Lissu aachiwe huru kwa kuwa kesi yake haikamiliki, Mwenyekiti Taifa wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mary Chatanda, amemtaka awe balozi wa kuhimiza viongozi na wananchi kutii sheria za nchi ili kuepuka kuingia mikononi mwa vyombo vya sheria.
Wiki iliyopita kupitia akaunti yake ya Mtandao wa X (zamani Twitter), Tibaijuka, ameandika: “Hekima na busara iliyokufanya kutangaza sera ya 4Rs mara ulipoingia madarakani ikuongoze tena katika jambo hili. Simulizi hizi za kutisha za vyombo vya habari vya kimataifa zinaibua hisia kali hasa kwa vijana hata wazee tumekumbushwa kadhia ya Operesheni Sogeza iliyounda vijiji vya ujamaa mwaka 1974 hadi 1976. Taarifa hizi zinaathiri kikubwa taswira ya taifa letu na masilahi yake.
“Athari ni kubwa. Tutafute mwafaka kupitia uwajibikaji na maridhiano. Tuwe na hofu ya Mungu na kutambua miujiza yake mfano wa risasi 16 kushindwa kukomesha uhai ingawa maumivu ni makubwa. Tutubu na kusali kuliombea taifa letu na kila mtu kwa imani yake.”
Kutokana na andiko hilo, Chatanda, akaibuka wiki iliyopita na kusema kwamba nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria. Pia ni vema mahakama iachwe ifanye kazi yake ili haki itendeke.
“Tusiruhusu utamaduni wa jambo linapokuwa mahakamani tuanze kumshinikiza Rais aingilie kati na kulimaliza. Tuiache mahakama ifanye kazi yake na itakapothibitika mtuhumiwa hana hatia ataachiwa huru,” amesema.
Pia amesema Tanzania ni huru, yenye mamlaka kamili na inaendesha mambo yake kwa mujibu taratibu zilizopo na vyombo vya habari vya kimataifa vinapaswa kuheshimu taratibu za uendeshaji wa nchi na mashauri ya kisheria.
“Tusiruhusu kila kinachoandikwa katika vyombo vya habari vya kimataifa kikayumbisha na kusababisha kuacha kusimamia sheria za nchi, ni lazima tuheshimiane linapokuja suala la utii wa sheria za nchi,” amesema.
Hivi karibuni, Jumuiya ya Madola (CW) imetoa mapendekezo ya kuitaka serikali kutafuta ufumbuzi wa kisiasa na kisheria kumaliza kesi inayomkabili Lissu.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa CW na Rais wa zamani wa Malawi na Mjumbe Maalumu wa jumuiya hiyo, Lazarius Chakwera, aliyeteuliwa kupatanisha mivutano ya kisiasa na kuwezesha mazungumzo ya kitaifa kutokana na vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.



