Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amewataka wananchi kutumia fursa ya Hewa ya Ukaa kwa kuzingatia mwongozo uliowekwa na Serikali ili kujiongezea kipato kupitia uhifadhi wa misitu na mazao, sambamba na kuchangia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Masauni alitoa rai hiyo Julai 21, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika wilaya za Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, akisema Serikali imeboresha uratibu wa biashara hiyo ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa njia halali na endelevu.
Alisema hapo awali hakukuwa na kanuni wala mwongozo wa biashara ya hewa ya ukaa, lakini kwa sasa Serikali imeweka utaratibu utakaowawezesha wananchi kupata elimu kupitia wataalamu wa halmashauri na kutumia rasilimali walizonazo, ikiwemo misitu na migomba, kujiongezea kipato.
Aidha, alisema biashara ya hewa ya ukaa ni mfumo wa soko la kimataifa unaolenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi zinazochangia ongezeko la joto duniani kwa kuthamini shughuli za uhifadhi wa misitu, upandaji miti na mifumo mingine inayopunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
“Mabadiliko ya tabianchi yameleta fursa ya biashara ya hewa ya ukaa kupitia Mkataba wa Paris, nchi zenye rasilimali za asili zinaweza kunufaika kwa kuhifadhi misitu na mazingira, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hii kujiletea maendeleo,” alielezea Masauni.
Alisisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na kukemea ukataji holela wa miti kwa ajili ya kuni, akiwataka wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi ili kunufaika na fursa zinazotokana na biashara ya hewa ya ukaa.
Vilevile, Masauni aliwaasa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema mkoa unaendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali za maendeleo, hususan kilimo na uwekezaji wa viwanda.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano idadi ya viwanda imeongezeka kutoka 1,367 hadi 1,722, ambapo viwanda 457 ni vikubwa na vya kati, huku viwanda 269 vikijengwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kuifungua Rufiji na Mkoa wa Pwani kwa ujumla,” alieleza Kunenge.
Kunenge pia alisema Mkoa wa Pwani umeendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu baada ya kuingia kwenye kumi bora kitaifa katika matokeo ya Kidato cha Sita kupitia shule nne.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, alisema wilaya inaendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia upandaji wa miti, ambapo mwaka huu wamepanda miche mbalimbali pamoja na miche milioni 1.5 ya mikorosho.
Alisema korosho ni zao kuu la biashara wilayani humo na kwa sasa wakulima wanaendelea na shughuli za palizi.
Kuhusu mapato ya ndani, Komba alisema halmashauri imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi bilioni 6.7 hadi bilioni 11.6, sawa na asilimia 171 ya lengo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, alimpongeza Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengerwa, kwa juhudi zake za kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo, akisema Rufiji ya sasa imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hususan katika sekta ya miundombinu.
Katika ziara hiyo, Masauni aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule mpya pamoja na nyumba ya mwalimu katika Kijiji cha Umwe wilayani Rufiji, alikagua ujenzi wa Barabara ya Ikwiriri, akazindua jengo la huduma kwa waraibu wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga na kuweka jiwe la msingi la jengo la ghorofa katika Shule ya Msingi Mwandege.





