Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Katavi

Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta za elimu, afya na kuboresha mazingira ya biashara ili kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Arthur Nanauka, akiwa Mpanda Mkoani Katavi ambako ameanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tano kwa lengo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kusikiliza changamoto za wananchi.

Akizungumza na wananchi na wafanyabiashara katika Soko Kuu la Mpanda, Mhe. Nanauka amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia uboreshaji wa mazingira ya biashara na sera za uwezeshaji kiuchumi.

Amesema hatua hizo zinakwenda sambamba na utoaji wa mikopo nafuu kwa wananchi, hususan vijana, wanawake na wenye ulemavu ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali zitakazowaletea maendeleo.

Katika kuimarisha ajenda ya maendeleo ya vijana, Mhe. Nanauka amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya vitendo na mafunzo ya ufundi stadi ili kuwajengea vijana ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwawezesha kujiajiri. “Katika kufanikisha hilo serikali inaendelea kuanzisha na kuendeleza vyuo maendeleo ya wananchi kwasababu ya mchango wake mkubwa katika kuzalisha nguvu kazi yenye maarifa na stadi zinazohitajika katika sekta mbalimbali za uzalishaji” ameongeza Nanauka.

Waziri Nanauka pia ametumia ziara hiyo kuwataka watumishi wa umma kuendelea kuzingatia uwajibikaji, uadilifu, weledi, na matumizi sahihi ya rasilimali za umma, akisema kuwa huo ndio msingi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.

Akihitimisha ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Waziri Nanauka amezungumza na vijana na kuwaeleza mikakati ya Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili, hususan ukosefu wa ajira na upatikanaji wa mitaji. Aidha, amewataka vijana kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Serikali katika ujasiriamali, mafunzo ya ufundi stadi, mikopo na programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi ili kujijengea kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.

Naomi Kagumba na Yunus Mrisho wanaosoma Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya wamefurahishwa na ujio wa ziara hiyo na kutoa ombi la kupatiwa Mikopo ili Waweze kujiajiri na kuajiki wengine kwani wamehitimu kozi ya upishi.