Wanafunzi wa shule za sekondari nchini wamehimizwa kuwekeza zaidi katika masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati (STEM) ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za ufadhili wa masomo (scholarship) zinazotolewa na Serikali.

Rai hiyo imetolewa Julai 23, 2026, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar alipokuwa akikagua mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji wa masomo ya sayansi katika Shule ya Sekondari Bustani Wilaya ya Rombo pamoja na Shule ya Sekondari Kisam, Wilaya ya Moshi Vijijini.

Akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule hizo, Dkt. Omar amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa kujenga maabara za kisasa zenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi wengi pamoja na kuzipatia vifaa muhimu vya mafunzo ya vitendo.

“Tumieni vyema maabara hizi kwa kujifunza kwa bidii masomo ya sayansi ili mnufaike na fursa za scholarship zinazotolewa na Serikali,” amesema Dkt. Omar.

Katika ziara hiyo, Dkt. Omar pia alikagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Mbomai iliyopo Wilaya ya Rombo pamoja na mradi jengo la TEHAMA na maktaba katika Shule ya Sekondari Mashati. Miradi yote imejengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka TEA CPA Mwanahamis Chambega amesema, zaidi ya shilingi milioni 540 zimetumika kukamilisha miradi hiyo, ikiwemo ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Mbomai, maabara mbili za sayansi katika Shule za Sekondari Kisam na Bustani pamoja na jengo la TEHAMA na maktaba katika Shule ya Sekondari Mashati.