Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wiki hii mjadala wa Katiba Mpya umepata afya mpya baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na vyama 18 vya siasa nchini. Mkutano huu, ukiuangalia kwa umakini, ni mwendelezo wa njia aliyoahidi kuifuata Rais Samia katika kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya aliposema, tujenge maridhiano kwanza. Hoja hii ni ya msingi. Ni vigumu kutunga Katiba Mpya kama pande zote za kisiasa hazina malengo yanayofanana.
Sitanii, neno maridhiano naona kuna watu linaelekea kuwakera. Binafsi naomba tuliite kwa jina lolote, lakini mwisho wa siku tuwe na nafasi ya kukaa kama taifa na kuzungumza. Wakatoliki wanajua kwamba Agano la Kale lilihamasisha falsafa ya jino kwa jino. Agano Jipya likaja na amri kuu ya upendo. Palipo na upendo, mipango hupangika na kusonga mbele kwa ufasaha.
Katiba ni moyo wa taifa. Ndiyo inayoelekeza namna mamlaka yanavyopatikana, haki za wananchi zinavyolindwa na wajibu wa kila mmoja unavyotekelezwa. Kwa sababu hiyo, Katiba Mpya haiwezi kuwa matokeo ya msukumo wa kisiasa wa muda mfupi, bali lazima iwe zao la mazungumzo, maridhiano na ushirikishwaji wa Watanzania wote.
Wiki hii, Rais Samia Suluhu Hassan ameendeleza mjadala wa Katiba Mpya kwa kuweka bayana msimamo wake kwamba Tanzania itaandika Katiba Mpya katika kipindi chake cha uongozi, lakini kwa kufuata taratibu, sheria na kanuni zilizopo nchini.
Kauli hiyo ya Rais Samia ni ya busara na inaonesha uongozi unaotanguliza utulivu wa taifa. Katiba ni mkataba wa wananchi, hivyo haiwezi kujengwa juu ya mazingira ya kutoaminiana. Lazima kwanza ijengwe misingi ya maelewano ndipo mchakato wa kuandika Katiba Mpya uweze kuzaa matunda yanayokubalika kwa wengi.
Hivi karibuni, Makamu wa Rais, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwahamasisha Watanzania kuendelea kudai Katiba Mpya. Kauli hiyo imeonesha kuwa uongozi wa juu wa nchi unatambua umuhimu wa kuwa na Katiba inayokidhi mahitaji ya wakati huu.
Sitanii, ni jambo la kupongezwa kwamba Rais Samia amekutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa. Hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kusikiliza mawazo tofauti badala ya kuyapuuza. Demokrasia yenye afya hujengwa kwa mazungumzo, si kwa kufungiana milango. Kadiri wadau wengi wanavyoshirikishwa, ndivyo Katiba Mpya itakavyokuwa na uhalali mkubwa mbele ya wananchi.
Jambo lingine la kupongezwa ni kauli ya Rais Samia kwamba maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar kati ya CCM na ACT Wazalendo yanapaswa kuwa nguzo ya maridhiano kwa Tanzania nzima. Huo ni mtazamo wa kiuongozi unaotambua kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuvunja mshikamano wa taifa. Badala yake, zinapaswa kuwa fursa ya kujenga maelewano yanayolinda amani, umoja na maendeleo ya Watanzania wote.
Historia inaonesha kuwa mataifa yaliyofanikiwa kufanya mabadiliko makubwa ya kikatiba kwa utulivu ni yale yaliyoweka mbele mazungumzo na kujenga imani kati ya wadau. Maridhiano yanawapa wananchi nafasi ya kusikilizana, kuheshimiana na kukubaliana kuhusu aina ya taifa wanalolitaka kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Katiba inayozaliwa katika mazingira hayo huwa na nguvu ya kudumu kwa sababu huakisi makubaliano mapana ya jamii.
Kwa msingi huo, msimamo wa Rais Samia haupaswi kutafsiriwa kama kuchelewesha Katiba Mpya, bali kama kuhakikisha mchakato wake unakuwa imara, jumuishi na wenye kukubalika. Kuandika Katiba Mpya ni muhimu, lakini muhimu zaidi ni kuhakikisha Katiba hiyo inatokana na maridhiano ya kweli na inakuwa mali ya Watanzania wote, si ya kundi au upande mmoja wa kisiasa.
Sitanii, Watanzania wana kila sababu ya kuunga mkono mwelekeo huu. Taifa letu limejijengea sifa ya kulinda amani na kutatua changamoto zake kwa mazungumzo. Ikiwa maridhiano yataendelea kupewa nafasi, na taratibu za kisheria zikaheshimiwa, hakuna shaka kwamba Tanzania inaweza kupata Katiba Mpya yenye kuimarisha demokrasia, utawala wa sheria na mshikamano wa kitaifa. Huo ndio urithi unaoweza kuendelea kuifanya Tanzania kuwa mfano wa utulivu, umoja na siasa za maridhiano barani Afrika.
Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827

