Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali imewakumbusha wadau wote nchini wanaohusika na uingizaji, uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuwa katazo hilo bado lipo na kuwataka wananchi kufuata wajibu huo na kutekeleza kama ilivyo kwa serikali inayo wajibu wa kusimamia utekelezaji wa zuio hilo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wakati wa Mkutano wa Wadau Kuhusu Udhibiti wa Taka za Plastiki Nchini, kilichofanyika jijini Dar es Salaa, Agosti 4, 2026.

Waziri Masauni  ambaye aliongozana na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga amesisitiza uwepo wa zuio hilo akieleza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuendelea kutekeleza zuio hilo.

“Zuio la watumia mifuko ya plastiki liko palele, madhumini ya zuio yalitokana na madhara ya kiafya na kimazingira hivyo jambo hili bado linaendelea kusimamiwa,” amesema.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara wameamua kufanya kazi kwa pamoja kwasimamia sera isilete mkwamo kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga amesema Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara yake zinategemeana katika utekelezaji wa majukumu yake ndio maana wamekutana na kuona namna gani ya kukabilina na jambo hilo.

Amesema suala la taka za plastiki lina taswira ya uchumi na wadau wake wametofautiana kulingana na matumizi ndio maana linatamwa kwa namna ya kipekee ili kulinda mazingira pamoja na viwanda vilivyopo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe, Albert Msando ameahidi kushirikiana na wakuu wengine wa wilaya katika kusimamia maelekezo ya Serikali hasa eneo la uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Ikumbukwe mwaka 2019, Serikali ilipiga marufuku uingizaji, uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kupitia Tangazo la Serikali Na. 394 la mwaka 2019.

 Aidha, mwaka 2022 Serikali ilipanua wigo wa katazo kwa kupiga marufuku matumizi ya lakiri za plastiki kwenye vifuniko vya chupa za maji na vinywaji kupitia Tangazo la Serikali Na. 291 la mwaka 2022. Tathmini ya miaka mitano (2019-2025) ya utekelezaji wa katazo inaonesha kuwa Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kusitisha uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya mifuko 3 ya plastiki iliyokuwa chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira nchini.