SHIRIKA la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limesema linaendelea kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kupata masoko kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, maabara za ubora na suluhisho za nishati.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, Mtafiti na Mtaalam wa Teknolojia za Nishati wa TIRDO, Augustino Masse, alisema shirika hilo limebaini fursa kubwa katika mazao yanayoharibika kwa haraka kama matunda na mbogamboga kwa kuyaongezea thamani kupitia teknolojia ya kuyakausha kwa gharama nafuu.
Alisema teknolojia hiyo inawawezesha wakulima kuhifadhi mazao kwa muda mrefu, kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna na kuongeza nafasi ya kuyafikia masoko yenye tija.
Masse alisema TIRDO pia imejikita katika kuboresha matumizi ya nishati kwenye uzalishaji kwa kuhakikisha viwanda vidogo na vya kati vinatumia nishati kwa ufanisi, hatua inayosaidia kupunguza gharama za uzalishaji huku ikiongeza tija.
“Kadri tunavyopunguza matumizi ya nishati au kutumia nishati kwa ufanisi, ndivyo tunavyopunguza gharama za uzalishaji na kuongeza uwezo wa wazalishaji kushindana sokoni,” alisema.
Aidha, alisema ubora wa bidhaa ni jambo la msingi katika kupata masoko, hivyo TIRDO ina maabara za kisasa zinazopima ubora wa bidhaa na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wazalishaji kuhusu hatua wanazopaswa kufuata ili bidhaa zao zikidhi viwango vinavyohitajika.
Kwa upande wa utunzaji wa mazingira, Masse alisema mabaki ya mazao ya kilimo ambayo mara nyingi huchukuliwa kuwa taka yanaweza kubadilishwa na kuwa mkaa mbadala, hivyo kutoa chanzo kingine cha nishati badala ya kuyachoma au kuyatupa.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza thamani ya mabaki ya mazao, kulinda mazingira na kuwapatia wakulima fursa ya kuongeza kipato.
Pia alisema TIRDO inaendelea kutekeleza jukumu la kuibua na kulea wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia mbalimbali nchini.
Alibainisha kuwa katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu, TIRDO imemshirikisha kijana mbunifu aliyebuni bidhaa inayojulikana kama Afro Hill, ambayo inalenga kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya zinazohusiana na homa ya ini.
Masse aliwataka wananchi, wakulima na wajasiriamali kutembelea banda la TIRDO lililopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kujifunza teknolojia mbalimbali zinazoweza kuongeza thamani ya mazao, kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.


