Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imewataka wawekezaji binafsi na taasisi mbalimbali nchini kutumia fursa zinazotolewa kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuwekeza katika ujenzi wa nyumba, majengo ya umma na makazi ya kisasa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora na kuharakisha maendeleo ya miundombinu nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, baada ya kutembelea banda la TBA katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Malecela Nzuguni, jijini Dodoma.Amesema Serikali imefanya maboresho ya sheria na kanuni zinazoiongoza TBA ili kuipa mamlaka mapana ya kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua itakayowezesha taasisi hiyo kuvutia mitaji na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma.

Dkt. Msonde amesema tangu kuanzishwa kwake, TBA imeendelea kutekeleza kwa ufanisi jukumu la kujenga na kusimamia majengo ya Serikali kwa viwango vya juu vya ubora, huku ikichangia kupunguza gharama za ujenzi na kuhakikisha usalama wa miundombinu ya umma. Alisema majengo mengi ya Serikali yaliyopo nchini ni ushahidi wa uwezo na weledi wa taasisi hiyo katika sekta ya ujenzi.

Ameongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, TBA sasa ina nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika kutatua changamoto ya makazi kwa kujenga nyumba bora kwa gharama nafuu. Alisema taasisi hiyo inaweza kubuni na kutekeleza miradi ya makazi inayokidhi mahitaji ya wananchi wa kipato cha chini na cha kati, huku ikitumia maeneo yake ya kimkakati kuvutia uwekezaji na kuendeleza miradi ya kisasa.

Dkt. Msonde, amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kupitia TBA utaongeza uwekezaji, ajira na kuchochea ukuaji wa sekta ya ujenzi, huku ukiwezesha ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma, makazi ya biashara na miradi mingine ya maendeleo. Amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa hizo mapema kwa kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji na milango iko wazi kwa wote wenye nia ya kushirikiana na TBA.

Aidha, Dkt. Msonde ameipongeza TBA kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini, akisema utendaji wake umeendelea kuijengea Serikali imani kutokana na ubora wa kazi zake. Alisisitiza kuwa matarajio ya Serikali ni kuona taasisi hiyo ikitumia kikamilifu mamlaka mapya iliyopewa kupanua wigo wa huduma, kuongeza miradi ya kimkakati na kuwa chachu ya kuvutia uwekezaji utakaobadilisha sekta ya makazi na miundombinu nchini.