Na Mwandishi Wetu, Tabora

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kurahisisha upatikanaji wa Alama ya Ubora kwa kuanzisha mfumo wa kidijitali unaowezesha wajasiriamali na wazalishaji kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kuongeza idadi ya bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Ipuli, Manispaa ya Tabora, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Bw. Hamis Seleleko, amesema maboresho hayo yameondoa changamoto zilizokuwepo awali ambapo waombaji walilazimika kuandika barua na kufika katika ofisi za TBS kuomba huduma hiyo.

Amesema kwa sasa mwombaji anaingia kupitia tovuti ya TBS, anajisajili kwenye mfumo, anajaza taarifa za bidhaa anayokusudia kuipatia Alama ya Ubora na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika bila kulazimika kufika ofisini.

“Baada ya maombi kuwasilishwa, sisi tunayapokea moja kwa moja kupitia mfumo na kuanza kuyafanyia kazi. Kwa Kanda ya Magharibi, ofisi yetu ipo Kigoma, hivyo tuna uwezo wa kuwafikia waombaji waliopo Tabora na maeneo mengine kwa haraka endapo watakuwa wametimiza vigezo vya kupata Alama ya Ubora,” amesema Seleleko.

Ameongeza kuwa matumizi ya mfumo wa kidijitali yameongeza ufanisi wa utoaji huduma, kupunguza muda wa kushughulikia maombi na kuwahamasisha wazalishaji wengi zaidi kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vinavyohitajika.

Wakati huohuo, baadhi ya wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo wameeleza kuwa elimu wanayoendelea kuipata kutoka TBS imewasaidia kutambua umuhimu wa Alama ya Ubora katika kuongeza ushindani wa bidhaa zao na kupanua masoko.

Mmoja wa wajasiriamali hao amesema kupata Alama ya Ubora ya TBS kulikuwa ndoto ya muda mrefu, akieleza kuwa msukumo mkubwa ulitokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipowatembelea katika Maonesho ya Sabasaba mwaka 2021 na kusisitiza umuhimu wa bidhaa zao kuwa na nembo ya TBS.

Amesema baada ya kupata Alama ya Ubora, tayari wameanza kuona matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kuvutia mwekezaji kutoka India anayehitaji tani 10 za asali kutoka Tanzania.

“Mahitaji hayo ni makubwa kwa mjasiriamali mmoja, lakini kupitia ushirikiano wetu na kuzingatia viwango vya TBS tunaweza kuzalisha kwa ubora unaotakiwa na kunufaika na masoko ya kimataifa,” amesema.

Wajasiriamali hao wamewataka wazalishaji wengine nchini kutumia fursa ya huduma zinazotolewa na TBS ili kuongeza thamani ya bidhaa zao, kujenga imani kwa walaji na kufungua masoko mapya ya ndani na nje ya Tanzania.