▪️Watuhumiwa 14 wakamatwa na tuhuma za utoroshaji madini
▪️Waigeuza nyumba ya kupanga kama soko
▪️Waziri Mavunde aelekeza uchunguzi kuwabaini na kukamata wahusika zaidi
▪️Mgeni mmoja kutoka nje ya nchi ahusishwa na utoroshaji
▪️Madini,fedha na vitendea kazi vyashilikiwa na serikali
Ikiwa ni sehemu ya usimamizi thabiti wa sekta na kuhakikisha Serikali inapata mapato yake ipasavyo kupitia mfumo rasmi wa masoko ya madini nchini, soko bubu la madini lagunduliwa jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 09 Agosti, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam na kubainisha kuwa zaidi ya watuhumiwa 14 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utoroshaji wa madini na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria hivi karibuni.
“Hawa wenzetu pamoja na Serikali kuwezesha masoko na vituo vya ununuzi vilivyosambaa Nchi nzima, wao wameona waje kupanga nyumba na kuigeuza soko la madini ambapo ni kinyume na Sheria.
Natoa rai kwa wenye nyumba wote kuhakikisha wanafahamu shughuli za msingi za wapangaji wao ili kutojiingiza kwenye matatizo haya.
Tutafanya ukaguzi maalum kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam na mikoa mingine kubaini hizi nyumba zinazotumika kama soko la madini na kuwa chanzo cha utoroshaji madini”Alisema Mavunde
Aidha, Waziri Mavunde amesema kwa taarifa za awali, raia mmoja wa kigeni anahusishwa na kitendo hicho cha kuwezesha utoroshaji wa madini nje ya mfumo rasmi na amedhibitiwa.
Vilevile, Mhe. Mavunde ameelekeza vyomba vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wote kwenye mnyororo huo wa vitendo vya utoroshaji wa madini.
Madini gram 174 yaliyokutwa katika soko hilo bubu pamoja na mashine mbili za XRF aina ya NITON DXL 800, Mizani ya kupimia uzito, Mitungi ya gas, vyungu vya kuchomea dhahabu, borax, pipeza gas, legis za kutengenezea umbo la dhahabu Pamoja na jumla ya pesa taslimu TZS. 54,705,000 vyote vinashikiliwa na serikali.







