Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeanza kuweka mfumo wa kamera za usalama barabarani ili kuimarisha utii wa sheria, kurejesha nidhamu na kudhibiti ajali zinazotokana na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Agosti 2026, alipokutana na Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Kitaifa, iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Machano Othman Said, Ikulu Zanzibar.
Amesema utekelezaji wa mfumo huo umeanza katika Mkoa wa Mjini Magharibi na utaendelea kuimarishwa na kupanuliwa katika maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini, kwa lengo la kuongeza usalama wa madereva, waendesha vyombo vya usafiri pamoja na watembea kwa miguu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha vituo vya mafunzo ya amali na kufanya mageuzi katika elimu ya ufundi ili kuwapatia vijana ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kujiajiri, kuajiriwa na kuwa na ushindani katika soko la ajira.
Kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa, amesema Serikali inaendelea kuweka bei elekezi na kusimamia utekelezaji wake, huku akiwataka wafanyabiashara kuzingatia viwango vilivyowekwa kwa lengo la kulinda maslahi ya wananchi na kupunguza gharama za maisha.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewataka wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi kuhakikisha mahitaji ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa katika majengo ya umma na binafsi, ili kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi na bila vikwazo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Machano Othman Said, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa maono na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo, na kueleza kuwa Kamati itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha maendeleo na kukuza uchumi wa Zanzibar.









