Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mvua inaponyesha, wengine huona neema; wengine huona hatari. Kwa mkulima, tone la kwanza linaweza kuwa mwanzo wa msimu wa matumaini. Kwa mfugaji, linaweza kumaanisha malisho na maji tele. Kwa mji, mvua hiyo hiyo inaweza kuwa chanzo cha mafuriko, uharibifu wa miundombinu na kusimama kwa shughuli za kiuchumi. Hapo ndipo tunapopaswa kuelewa jambo moja muhimu: mvua yenyewe si adui; kutokuwa tayari kwa mvua kunaweza kuwa tatizo.
Mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli wa Oktoba hadi Desemba 2026 uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) chini ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Ladislaus Benedict Chang’a unapaswa kuwa mwongozo wa maamuzi kwa jamii na sekta mbalimbali. Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani, huku hali ya El Niño ikitarajiwa kuchangia mwenendo wa msimu huo.
Mvua zinatarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo mwishoni mwa Septemba na mapema Oktoba, huku ongezeko la mvua likitarajiwa hasa mwezi Novemba. Aidha, mvua zinaweza kuendelea hadi Januari 2027.
Chang’a ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC) anasema kuwa hii si taarifa ya kuogopesha jamii bali ni taarifa ya kusaidia kujiandaa mapema kutoka kwenye utabiri hadi kwenye hatua nyingine.

“Changamoto kubwa si kupata taarifa ya hali ya hewa pekee; changamoto ni kuigeuza taarifa hiyo kuwa uamuzi na hatua.
“Mkulima anayejua kuwa mvua zinatarajiwa kuwa nyingi anaweza kuchagua muda sahihi wa kupanda, mbegu zinazofaa na mbinu za kuzuia maji kutuama shambani. Anaweza kuimarisha mifereji, kupunguza mmomonyoko wa udongo na kupanga namna bora ya kuvuna na kuhifadhi mazao kabla hayajaharibiwa na unyevu.
Kwa hiyo, utabiri wa hali ya hewa haupaswi kubaki kwenye ofisi za wataalamu. Unapaswa kufika shambani na kutumika katika kufanya maamuzi” anasema.
Hata hivyo anasema kuwa maji mengi ni neema yenye masharti, mvua za kutosha zinaweza kuongeza unyevu wa udongo, kujaza mabwawa na mito, kuongeza upatikanaji wa maji kwa mifugo na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Lakini maji yakizidi, neema inaweza kubadilika kuwa hasara. Mafuriko yanaweza kuharibu mashamba, barabara, madaraja, nyumba na miundombinu ya maji. Udongo uliolowa kupita kiasi unaweza kuongeza mmomonyoko na kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao. Katika maeneo ya uchimbaji madini, mvua nyingi zinaweza kuongeza hatari ya maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa mashimo yasiyo imara.
MIJI INAPASWA KUJIANDAA
Chang’a anasema kuwa katika maeneo ya mijini, mvua kubwa inaponyesha, mifereji iliyozibwa na taka inaweza kugeuka kuwa chanzo cha mafuriko. Maandalizi hayapaswi kuanza baada ya maji kuingia ndani ya nyumba; yanapaswa kuanza wakati anga bado likiwa tulivu.
Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapaswa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji, kutambua maeneo hatarishi na kuelimisha wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa. Kuimarisha kamati za maafa katika ngazi za jamii pia ni hatua muhimu katika kupunguza madhara.

USALAMA WA CHAKULA UNAANZA NA TAARIFA
Anasema kuwa mvua za Vuli 2026 zinaweza kuwa fursa kwa uzalishaji wa chakula, lakini pia zinaweza kuleta changamoto za magonjwa ya mimea, mafuriko na upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Hivyo, mkakati wa usalama wa chakula haupaswi kuishia kwenye kuongeza uzalishaji. Lazima uzingatie pia kuhifadhi kile tulichozalisha.
Uvunaji kwa wakati, maghala salama, usafirishaji uliopangwa na matumizi ya taarifa za hali ya hewa vinaweza kupunguza upotevu wa mazao. Kwa maneno mengine, tone la mvua linapaswa kutafsiriwa kuwa chakula mezani, si hasara ghalani.
MIGUGO, UVUVI NA WANYAMAPORI
Anaongeza kuwa mvua nyingi zinaweza kuongeza malisho na upatikanaji wa maji kwa mifugo, lakini pia zinaweza kuleta mazingira yanayofaa kwa baadhi ya magonjwa na wadudu wanaosambaza magonjwa.
Kwa wavuvi na wakulima wa mwani, mabadiliko ya mazingira ya maji yanaweza kuathiri shughuli zao. Hivyo, maamuzi kuhusu shughuli za uvuvi na maeneo ya uzalishaji yanapaswa kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa.
Kwa upande wa wanyamapori, maji mengi yanaweza kubadilisha mienendo ya wanyama na kuwafanya kuelekea maeneo ya jamii. Hali hiyo inaweza kuongeza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Suluhisho si kusubiri mgogoro utokee ni vyema kuimarisha ufuatiliaji, kutoa taarifa mapema na kuchukua hatua kabla hali haijawa mbaya.
MIUNDOMBINU NA USAFIRISHAJI
Ramadhan Omary ambaye ni mchambuzi wa hali ya hewa kutoka TMA, anasema kuwa mvua kubwa zinaweza kuathiri barabara, madaraja, reli, bandari na viwanja vya ndege. Mmomonyoko wa udongo na mafuriko vinaweza kuvuruga usafirishaji wa watu na bidhaa, kuongeza gharama za uendeshaji na hata kuhatarisha maisha.
“Kwa hiyo, taarifa ya hali ya hewa inapaswa kuwa sehemu ya mipango ya usafirishaji. Ukaguzi wa madaraja, mifereji na maeneo hatarishi kabla ya mvua kubwa si gharama isiyo ya lazima; ni uwekezaji katika usalama wa watu na mali” anasema.

AFYA YA JAMII NA HALI YA HEWA
Pia anasema kuwa mafuriko yanaweza kuchafua vyanzo vya maji na kuharibu mifumo ya maji taka. Maji yaliyotuama yanaweza pia kuongeza mazalia ya mbu na hivyo kuongeza hatari ya baadhi ya magonjwa.
“Kwa hiyo, maandalizi ya sekta ya afya yanapaswa kuanza kabla ya mlipuko wa ugonjwa. Maji salama, usafi wa mazingira, dawa, vifaa tiba na mipango ya kuhakikisha huduma za afya zinaendelea wakati wa maafa ni muhimu” anaongeza.
EL NINO SI HUKUMU
Anasema kuwa hali ya El Niño inayotarajiwa kuchangia mwenendo wa msimu huu haipaswi kuwa sababu ya kueneza hofu. Inapaswa kuwa wito wa kuongeza umakini na maandalizi.
“Jamii yenye taarifa inaweza kufanya maamuzi bora. Mkulima mwenye taarifa anaweza kupanga. Mji wenye taarifa unaweza kusafisha mifereji. Hospitali yenye taarifa inaweza kujiandaa. Msafirishaji mwenye taarifa anaweza kupanga ratiba. Serikali yenye taarifa inaweza kuelekeza rasilimali mapema.Hivyo, utabiri wa hali ya hewa ni kinga kabla ya janga.
SEKTA BINAFSI
Akizungumzia utabiri wa hali hewa, mfanyabiashara wa mahindi kutoka Kibaigwa mkoani Dodoma, Jonathan Kileo, anasema kuwa kwa mfanyabiashara, mvua zinaweza kuwa fursa au gharama. Uzalishaji unaweza kuongezeka, lakini mafuriko yanaweza kuvuruga minyororo ya usambazaji, kuharibu bidhaa na kuongeza gharama za uendeshaji.
“Hivyo, biashara zinapaswa kuwa na mipango ya dharura, bima, uhifadhi salama wa bidhaa na mifumo ya mawasiliano. Kutumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga biashara ni kujenga ustahimilivu wa kiuchumi.
“Lakini pia ni vyema utabiri utabiri wa hali ya hewa ambao hivi sasa umekuwa msaada mkubwa kwetu kutokana na tabiri kuwa na uhakika wa asilimia kubwa na kutusaidia sisi wafanyabiashara na wakulima na hata Serikali kujipanga pia” anasema.
Lakini pia mwananchi anahitaji kuelimishwa ni maeneo gani mvua kubwa itainyesha, madhara gani yanaweza kutokea na afanye nini kwani hapo ndipo taarifa ya hali ya hewa inapogeuka kuwa huduma kwa jamii kwa kusaidia wananchi kuchukua tahadhari lakini pia na taifa kiujumla.
KULINDA MAZINGIRA KABLA YA MAFURIKO
Msimu wa Vuli 2026 unatupa nafasi ya kufanya mambo tofauti kutumia taarifa kabla ya tukio, kuimarisha miundombinu kabla ya mvua, kulinda mazingira kabla ya mafuriko na kuelimisha jamii kabla ya taharuki.
Hatuwezi kuzuia mvua kunyesha. Lakini tunaweza kupunguza madhara yake kwa kusikiliza wataalamu, kufuatilia taarifa rasmi, kujiandaa mapema na kuchukua hatua sahihi.
Mvua ya Vuli ikifika, iwe chanzo cha uzalishaji, si chanzo cha maafa; iwe neema inayovunwa kwa maandalizi, si changamoto inayotushangaza.
Kwa sababu hatuwezi kuamua mvua inyeshe au isinyeshe.Lakini tunaweza kuamua jinsi tutakavyokabiliana nayo. Tahadhari leo, usalama wa kesho.

