Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameagiza Mamlaka na Taasisi zinazohusika kuchukua hatua za haraka kujiandaa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo, mara baada ya kupokea taarifa ya utayari na maandalizi ya Serikali kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu mvua za El- nino, katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza septemba 11,2026 Jijini Dar Es Salaam na Viongozi pamoja na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zilizochini ya Wizara hizo, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa taasisi zote zinazohusika, kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kuzuia au kupunguza athari zinazoweza kutokea kwa wananchi kufuatia ujio wa mvua hizo.
Pia amesisitiza umuhimu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kushirikishwa katika maandalizi hayo ili kuwa na nguvu kazi ya kutosha pamoja na kuimarisha uwezo wa Serikali wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana kwa haraka na athari zinazoweza kujitokeza.
“Ifanyike kampeni ya haraka, mikondo na mifereji ya maji izibuliwe, na barabara ziandaliwe,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Aidha, ameelekeza taka, tope na udongo unaotolewa baada ya kuzibua mitaro na mifereji katika maeneo mbalimbali kuondolewa mara moja na kutupwa katika maeneo yaliyotengwa, badala ya kuachwa kandokando ya barabara ambako unaweza kurejea kwenye mifereji wakati mvua zinapoanza.

Makamu wa Rais pia ameagiza mamlaka husika kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara, kuchukua hatua za haraka kusambaza vifusi vilivyorundikwa katika maeneo yenye shughuli za ujenzi, akisisitiza kuwa kazi hiyo haipaswi kusubiri hadi mvua zianze kunyesha kwani husababisha usumbufu na kero kwa wananchi.
Amesema katika maeneo yenye miradi ya ujenzi wa barabara ni lazima kuwe na mipango madhubuti itakayohakikisha barabara zinaendelea kupitika kwa urahisi na usalama, ili shughuli za ujenzi zisigeuke kuwa chanzo cha usumbufu au kuongeza athari kwa wananchi wakati wa mvua.
Katika kikao hicho, Makamu wa Rais alipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe; pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya.
Taarifa ziliyowasilishwa katika kikao hicho zimeeleza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kupitia Kamati ya Kitaifa iliyoundwa kuratibu hatua za kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua za El Niño.

Miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kufanya tathmini ya makazi yaliyopo mabondeni na maeneo mengine yenye hatari ya mafuriko, kuongeza elimu na tahadhari kwa umma, kufanya tathmini ya masoko na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, pamoja na kuendesha kampeni za usafi wa mazingira.
Hatua nyingine ni kuzibua mitaro, mifereji na mikondo ya maji, kulinda njia za asili za maji, kudhibiti maji taka na kufanya ukaguzi wa madaraja pamoja na miundombinu mingine muhimu ili kubaini maeneo yenye hatari na kuchukua hatua kabla ya mvua kuanza.
Serikali pia imeweka mkazo katika kuwa na mpango shirikishi wa dharura utakaowezesha Taasisi mbalimbali kuratibu hatua za uokoaji na utoaji wa huduma muhimu endapo kutatokea mafuriko au majanga mengine yanayohusiana na mvua hizo.


