Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma
Watumiaji wa huduma za maji, umeme, petroli na gesi asilia wametakiwa kufahamu haki na wajibu wao ili waweze kulinda maslahi yao, kupata huduma salama na kudai stahiki pale wanapokutana na changamoto.
Wito huo umetolewa Septemba 18, 2026, jijini Dodoma na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), wakati likitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha VETA Dodoma .
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa EWURA CCC, Amani Mbogo, amesema watumiaji wana haki ya kupata huduma za msingi kwa kuzingatia viwango vya ubora na bei zilizoidhinishwa na mdhibiti.
Amesema maji na nishati ni huduma muhimu katika maisha ya kila siku, hivyo mtumiaji anapaswa kupata huduma hizo kwa masharti yanayozingatia usalama, ubora na bei zinazotambuliwa kisheria.
“Mtumiaji ana haki ya kupata huduma ya msingi,maji na nishati ni huduma za msingi katika ustawi wa maisha ya binadamu na huduma hizi zinapaswa kuwa na bei nafuu kwa kuzingatia bei zilizoidhinishwa na mdhibiti,” amesema Mbogo.
Mbogo amesema miongoni mwa haki nyingine ni kupata usalama na faragha, akieleza kuwa mtumiaji anapaswa kupata huduma salama na kulindwa dhidi ya bidhaa, michakato au huduma zinazoweza kuhatarisha afya au maisha yake.
Amesema pia mtumiaji ana haki ya kupata taarifa sahihi na zinazojitosheleza kuhusu huduma anayotumia, ikiwa ni pamoja na taarifa kuhusu mabadiliko ya bei au kusitishwa kwa huduma kwa muda kutokana na matengenezo.
Kwa mujibu wa Mbogo, haki hiyo ni muhimu kwa sababu humwezesha mtumiaji kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma anayotumia.
Mbogo amesema mtumiaji ana haki ya kuchagua huduma kwa kuzingatia bei na ubora, akitoa mfano wa bidhaa za petroli ambapo mtumiaji anaweza kulinganisha bei katika vituo mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wa mahali pa kununua.
Amesema uchaguzi huo unapaswa kuongozwa na taarifa sahihi kuhusu huduma inayotolewa.
“EWURA CCC inaweza kumwakilisha mtumiaji ambaye hajui kusoma na kuandika, mgonjwa au mtu mzima sana. Tunachukua malalamiko yake na kumsaidia mtumiaji aweze kupata haki yake ya msingi,” amesema.
Kuhusu haki ya kudai fidia,Mbogo amesema mtumiaji pia ana haki ya kupata utatuzi wa madai na fidia pale inapobainika kuwa amepata hasara kutokana na mtoa huduma, kwa mujibu wa taratibu na masharti yanayohusika.
Ametoa mfano wa mtumiaji kupewa bili isiyo sahihi au kupata hasara inayohusishwa na huduma, akisisitiza kuwa suala hilo linaweza kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya uchunguzi na hatua stahiki.
Aidha, amesema watumiaji wana haki ya kuishi na kutumia huduma katika mazingira salama, ikiwemo kutoa taarifa kuhusu miundombinu hatarishi kama nguzo za umeme zilizoanguka, nyaya hatarishi, mabomba yaliyopasuka au majitaka yanayovuja.
Mbali na haki, Mbogo amesema mtumiaji anapaswa kufuata taratibu halali wakati wa kuomba kuunganishiwa huduma za maji au umeme, badala ya kutumia njia zisizo rasmi.
Mbogo amesema mtumiaji ana wajibu wa kutoa taarifa kwa mtoa huduma anapoona tatizo katika miundombinu ya huduma, hata kama tatizo hilo limetokea nje ya eneo analoishi.
Amesema taarifa kuhusu bomba lililopasuka, majitaka yanayovuja au nguzo ya umeme iliyoanguka inaweza kusaidia mtoa huduma kuchukua hatua mapema na kuzuia madhara zaidi.
“Mtumiaji akipita eneo fulani na kukuta majitaka yanamwagika, bomba limepasuka au nguzo ya umeme imeanguka, anapaswa kutoa taarifa kwa mtoa huduma. Wakati mwingine mtoa huduma anaweza kuwa hana taarifa kuhusu changamoto hiyo,” amesema.
Pamoja na hilo, watumiaji wametakiwa kutunza miundombinu ya huduma na kutoa taarifa pale wanapoona vitendo vya uharibifu, wizi au hujuma dhidi ya miundombinu ya maji na nishati.
Mbogo pia amesisitiza umuhimu wa mtumiaji kujielimisha kuhusu huduma anayotumia, ikiwemo namna ya kusoma mita, kutunza kumbukumbu za matumizi na kuzingatia masuala ya usalama.
Amesema EWURA CCC itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali jijini Dodoma na maeneo mengine ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika huduma za nishati na maji.
EWURA CCC ni baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za nishati na maji lenye jukumu la kuwakilisha na kutetea maslahi ya watumiaji katika huduma zinazodhibitiwa, zikiwemo maji, umeme, mafuta ya petroli na gesi asilia.



