Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwawezesha kunufaika na maeneo ya kimkakati yaliyowekezwa miundombinu, wakisema hatua hiyo inaweza kuongeza uzalishaji, usindikaji na biashara katika Mkoa wa Pwani.
Kauli hiyo imetolewa katika mjadala wa uwekezaji uliohusisha wadau mbalimbali wa biashara, ambapo baadhi ya washiriki walieleza changamoto wanazokutana nazo katika kupata maeneo ya kuendesha shughuli zao licha ya kuwepo kwa maeneo ambayo tayari Serikali imewekeza miundombinu.

Mkurugenzi wa kampuni ya Kipa Foods and General Supplies Limited, Bi Elly Palanjo ambaye anajihusisha na usindikaji wa mazao ya kilimo ikiwamo muhogo na mabaki yake kwa ajili ya chakula cha mifugo, alisema Pwani ina fursa kubwa za uwekezaji ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

Amesema baadhi ya maeneo ambayo Serikali imewekeza tayari yanaweza kutumika kuwawezesha wawekezaji wa ndani kuanzisha viwanda vya usindikaji na kuongeza thamani ya mazao.

“Kwa Mkoa wetu wa Pwani kuna fursa nyingi sana na bahati nzuri Serikali pia imewekeza katika baadhi ya maeneo. Lakini tunajiuliza tunawezaje kunufaika na maeneo hayo,”? amesema

Alitoa mfano wa eneo lililopo Mlandizi, akisema ni miongoni mwa maeneo yenye nafasi ya kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji kuongeza shughuli zao iwapo yatafunguliwa kwa utaratibu unaowahusisha wawekezaji wa ndani.

“Unaona eneo ambalo liko very strategic. Sisi kama wajasiriamali na makampuni ya kizawa tungepewa fursa ya ku-operate mle, nahisi ingekuwa rahisi zaidi,” amesema.

Alisema maeneo yenye miundombinu ya Serikali yanaweza kuwa na manufaa zaidi endapo yataunganishwa na shughuli za uzalishaji, usindikaji na masoko, badala ya kubaki bila kutumika kikamilifu.

Bandari kavu

Katika mjadala huo, mmoja wa washiriki kutoka Chama cha Wafugaji wa Kiluvya, Kibaha, alisema kundi lake linajihusisha na ufugaji wa ng’ombe pamoja na usindikaji wa maziwa wanayozalisha na yale wanayonunua kutoka kwa wafugaji wengine.

Amesema changamoto ya matumizi ya maeneo ya kimkakati inapaswa kuangaliwa kwa mtazamo mpana, hasa kutokana na nafasi ya Pwani katika shughuli za usafirishaji na biashara.

Alitaja Bandari Kavu ya Kwala kuwa miongoni mwa uwekezaji uliolenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani.

Kwa mujibu wake, ongezeko la vituo vidogo vya mizigo (ICDs) linapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia mpango mpana wa kiuchumi ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliowekwa katika miundombinu ya usafirishaji unatoa matokeo yaliyokusudiwa.

Amesema baadhi ya ICD zimejengwa katika maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa matumizi ya jamii, akitaka suala hilo liangaliwe katika muktadha wa mipango miji na maslahi mapana ya uchumi wa Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.

Matarajio ya Kigamboni
Mshiriki mwingine kutoka Estate Chamber Dar es Salaam alisema baadhi ya wananchi waliwekeza katika maeneo ya Kigamboni wakitarajia maendeleo makubwa kufuatia mipango ya Serikali ya kuendeleza eneo hilo.

Amesema matarajio hayo yalichochea baadhi ya watu kununua maeneo kwa kuamini kuwa maendeleo ya miundombinu yangeongeza fursa za biashara na uwekezaji.

“Watu walikimbilia kule kwenda kununua maeneo kwa matarajio kwamba Kigamboni italeta fursa, lakini mpaka leo tunaona hakuna ambacho kimeendelea kama tulivyotarajia,” amesema.

Alisema changamoto hiyo inaonyesha umuhimu wa kuwa na mipango ya uwekezaji inayokwenda sambamba na utekelezaji wa miundombinu na kuwapa wawekezaji taarifa sahihi kuhusu fursa zinazotarajiwa katika maeneo husika.

Mjadala huo umeibua hitaji la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutambua maeneo yenye uwezo wa kuzalisha thamani, kuongeza ajira na kuchochea biashara, huku uwekezaji ukiongozwa na mipango ya muda mrefu ya kiuchumi na matumizi bora ya ardhi.