Mawaziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho na Mheshimiwa Cristóvão Artur Chume, wamehitimisha rasmi Mkutano wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama kati ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo, uliofanyika jijini Dar es Salaam, umehitimishwa tarehe 7 Oktoba 2026 kwa kusainiwa kwa makubaliano mbalimbali yanayolenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji katika masuala ya ulinzi na usalama, hususan katika kulinda amani, utulivu na usalama wa wananchi wa nchi hizo mbili.
Mkutano huo wa saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama umelenga, miongoni mwa mambo mengine, kuendeleza na kuimarisha maono ya waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Samora Moisés Machel wa Msumbiji, ambao waliweka msingi imara wa uhusiano wa kihistoria, kidugu na kimkakati kati ya Tanzania na Msumbiji.
Maono hayo yanaendelea kuenziwa na kuendelezwa na viongozi wa sasa wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Chapo, kupitia kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.





