Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha utaalamu wa ndani katika fani ya uhandisi na kusaidia maendeleo endelevu ya viwanda nchini Tanzania kupitia uwekezaji katika kujenga uwezo wa kitaalamu na ushirikiano na vyuo vikuu pamoja na taasisi za mafunzo ya ufundi.

Dhamira hiyo ilielezwa wakati wa Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Uhandisi wa Mitambo na Viwanda (MIE 2026), uliofanyika mapema wiki hii katika Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zanzibar.

Mkutano huo, uliokuwa na kaulimbiu isemayo “Ubunifu wa Uhandisi kwa Mabadiliko Endelevu ya Viwanda kuelekea Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050,” uliwakutanisha watafiti, wahandisi, wanafunzi, viongozi wa sekta ya viwanda na watunga sera kwa ajili ya kubadilishana maarifa, kuonesha ubunifu wa kiteknolojia na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Sandra Suleiman wa EACOP alisisitiza umuhimu wa uwekezaji unaoendelea kufanywa na mradi huo katika fani za uhandisi wa mitambo na viwanda kupitia programu za kujenga uwezo na ushirikiano wa kimkakati na vyuo vikuu pamoja na taasisi za mafunzo ya ufundi.

Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa watu binafsi na taasisi, hatua itakayoiwezesha Tanzania kukuza utaalamu wa kiufundi unaohitajika kusaidia mageuzi ya sekta ya viwanda nchini.

“Uwekezaji katika kujenga uwezo wa wahandisi na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na vyuo vikuu pamoja na taasisi za mafunzo ya ufundi ni hatua muhimu katika kukuza utaalamu wa ndani na kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi wa kusaidia maendeleo ya viwanda nchini Tanzania,” alisema.

Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya sekta ya viwanda na taasisi za kitaaluma unatoa fursa ya kuunganisha maarifa ya darasani na mahitaji halisi ya kiutendaji katika sekta hiyo.

Ushirikiano huo pia huwasaidia wanafunzi na wataalamu kupata ujuzi unaoendana na vipaumbele vya maendeleo ya nchi.

Mkutano huo ulitoa jukwaa kwa wadau kujadili suluhisho za kihandisi zinazoweza kusaidia ukuaji wa viwanda, kuongeza tija na kuendeleza maendeleo endelevu kwa kuzingatia malengo ya muda mrefu ya Tanzania kupitia Dira ya Maendeleo ya 2050.

Ushiriki wa EACOP katika mkutano huo ulionesha msisitizo wa kampuni hiyo katika kukuza vipaji vya ndani vya uhandisi, kuendeleza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani na kuimarisha ubadilishanaji wa maarifa kati ya sekta ya viwanda na taasisi za mafunzo.

Kupitia juhudi hizo, kampuni inalenga kuchangia katika kujenga msingi imara wa ujuzi wa ndani na kuongeza uwezo wa taasisi za Tanzania kusaidia mahitaji yanayobadilika ya viwanda na miundombinu nchini.

EACOP imesisitiza kuwa kuendelea kuwekeza kwa watu, ujuzi wa kitaalamu na ushirikiano na taasisi ni muhimu katika kufanikisha mageuzi endelevu ya viwanda na kuhakikisha Watanzania wanakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika fursa za maendeleo ya nchi.