Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kutumia majengo na miundombinu ya kisasa iliyowekwa kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi badala ya kujikita katika kufurahia uzuri wa majengo hayo.
Profesa Kabudi aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Alisisitiza kuwa uwekezaji katika majengo na miundombinu ya Serikali unapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika utendaji wa watumishi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Alisema majengo ya kisasa pekee hayawezi kuleta mabadiliko yanayotarajiwa bila kuwapo kwa uwajibikaji, uadilifu, ubunifu, nidhamu ya kazi na uzalendo miongoni mwa watumishi wa umma.
“Majengo mazuri pekee hayatoshi, tunahitaji pia utendaji bora, nidhamu ya kazi na uzalendo ili wananchi waone matokeo ya uwekezaji huu kupitia huduma bora za Serikali,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, mazingira bora ya kazi yaliyowekwa na Serikali yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza ufanisi, kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Alisema kuwekwa kwa wizara na taasisi mbalimbali za Serikali katika eneo moja kutarahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, mawasiliano na ushirikiano baina ya taasisi, pamoja na kupunguza changamoto zinazotokana na ofisi kutawanyika katika maeneo tofauti.
Aidha, alisema barabara za lami zilizojengwa katika mji huo zitaboresha usafiri na mawasiliano, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuunganisha maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mji wa Serikali.
Aliongeza kuwa maendeleo ya Mtumba yanafungua fursa za kiuchumi kwa sekta binafsi na wananchi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafirishaji, malazi, biashara na huduma za kitaalamu.
Kutokana na hali hiyo, aliwahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika Mji wa Serikali na Dodoma kwa ujumla, akieleza kuwa ongezeko la shughuli za Serikali linaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Profesa Kabudi alisema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Mtumba ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na kuweka mazingira yatakayowezesha taasisi za Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine, wananchi, hususan wakazi wa Mkoa wa Dodoma, wamehimizwa kujitokeza kushuhudia uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba.
Taarifa iliyotolewa kuhusu shughuli hizo ilieleza kuwa upigaji fataki ulipangwa kufanyika usiku wa Oktoba 30, 2026, kuelekea uzinduzi huo.





