Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa viwango 3,901 vya bidhaa katika sekta mbalimbali na kutoa vyeti na leseni za ubora 3,940 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia mwaka 2021 hadi 2026.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TBS, Dkt. Ashura Katunzi wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili Hazina na waandishi wa habari pamoja na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa nchini, kuwawezesha wazalishaji kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa ambapo TBS, iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha sekta za viwanda na biashara, hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango, Sura ya 130.

“Katika kipindi hicho, shirika limeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma, kuimarisha ukaguzi wa bidhaa, kusajili bidhaa na maeneo ya biashara pamoja na kutoa elimu kwa wazalishaji na wadau wengine kuhusu masuala ya viwango na ubora” amesema.

Amesema kuwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma, TBS inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji na makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, unaojulikana kama Viwango House–Dodoma, wenye thamani ya Sh bilioni 24.7.

Pia, shirika linaendelea na ujenzi wa ofisi na maabara katika eneo la Kiseke, Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza, kupitia mradi wa Viwango House–Mwanza, unaokadiriwa kugharimu Sh bilioni 12.1.

Aidha, TBS ipo katika hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa ofisi na maabara nyingine jijini Arusha, zitakazojulikana kama Viwango House–Arusha.

“Maabara za Dodoma zinatarajiwa kuhudumia mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, wakati maabara za Mwanza zitahudumia mikoa sita ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.

“Uwekezaji huo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza gharama za upimaji, huku ukiongeza ufanisi katika upatikanaji wa majibu ya vipimo vya sampuli” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika hatua nyingine, Serikali kupitia TBS imetumia zaidi ya Sh bilioni 9.8 kuimarisha ofisi tisa za kanda pamoja na ofisi za mipakani, bandarini na viwanja vya ndege.

Ofisi hizo zinahusisha kanda za Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita, pamoja na maeneo mbalimbali ya kuingilia bidhaa nchini.

Uboreshaji huo umehusisha kuongeza ofisi, wafanyakazi na vitendea kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa sokoni na mipakani ili kupunguza uwepo wa bidhaa hafifu na kulinda afya na usalama wa walaji.

Viwango 3,901 vyatayarishwa

Katika kuwezesha biashara, TBS ina kamati za kitaalamu 117 zinazohusika na uandaaji wa viwango katika sekta mbalimbali, zikiwemo chakula, kemikali, uhandisi wa mitambo, umeme, ujenzi, nguo na ngozi, madini, mazingira na taaluma mtambuka.

Kamati hizo hushirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa kuandaa viwango, wakiwemo vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wafanyabiashara, wazalishaji, vyama vya walaji, bodi za kitaalamu, taasisi za udhibiti na watunga sera.

Kupitia mchakato huo, shirika limeandaa viwango 3,901 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuzingatia mahitaji ya soko.

Viwango hivyo vinatarajiwa kuwasaidia wazalishaji, wajasiriamali na watoa huduma kuboresha bidhaa zao ili zikidhi matakwa ya viwango vinavyotakiwa na kuongeza uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa. Aidha, TBS imetoa jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,940 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683.

Serikali imekuwa ikitenga zaidi ya Sh milioni 300 kila mwaka kwa ajili ya kutoa huduma za uthibitishaji wa ubora kwa wajasiriamali wadogo bila malipo.

Mpango huo unalenga kuwawezesha wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika, kuongeza imani ya walaji na kupanua fursa za kuuza bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

Bidhaa 9,731 zasajiliwa

Katika kulinda afya za walaji, TBS imeendelea kusajili bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo yanayohusika na uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa bidhaa hizo.

Katika kipindi hicho, jumla ya bidhaa 9,731 zilisajiliwa, huku maeneo 80,836 yakisajiliwa kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa bidhaa na mazingira ambamo zinashughulikiwa.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha udhibiti wa bidhaa zinazotumiwa na wananchi na kuhakikisha zinakidhi matakwa ya ubora na usalama.

Vilevile, shirika limeimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka mataifa ya nje ili kuzuia kuingia kwa bidhaa zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.

Kupitia mfumo wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja Tanzania, unaojulikana kama Pre-Shipment Verification of Conformity (PVoC), TBS ilikagua shehena 183,186 katika kipindi hicho.

Kwa upande wa ukaguzi wa bidhaa baada ya kufika nchini, kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI), shehena 426,842 zilikaguliwa.

Aidha, magari yaliyotumika 249,386 yalikaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Ukaguzi huo unalenga kuzuia Tanzania kuwa soko la bidhaa duni, kulinda afya na usalama wa watumiaji na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa mazingira.

Wadau 6,824 wapatiwa mafunzo

Katika kuongeza uelewa wa masuala ya viwango na ubora, TBS imetoa mafunzo kwa wadau 6,824, wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji.

Mafunzo hayo yalihusu masuala ya viwango, udhibiti wa ubora na mahitaji yanayotakiwa kuzingatiwa katika uzalishaji wa bidhaa.

Kupitia mafunzo hayo, wadau wanatarajiwa kuongeza uelewa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango, pamoja na kuimarisha ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Kwa ujumla, uwekezaji katika maabara, uimarishaji wa ofisi za kanda, uandaaji wa viwango, uthibitishaji wa bidhaa na utoaji wa mafunzo ni sehemu ya juhudi za TBS za kuimarisha ubora na usalama wa bidhaa nchini na kusaidia ukuaji wa sekta za viwanda na biashara.